Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na GEG wajumuika katika mradi kwa kuwezesha upatikanaji wa takwimu kuhusu misitu

Misitu inatoweka
World Bank/Curt Carnemark
Misitu inatoweka

FAO na GEG wajumuika katika mradi kwa kuwezesha upatikanaji wa takwimu kuhusu misitu

Tabianchi na mazingira

Shirika la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limezindua mradi mpya wa  dola milioni 7.1 unaosaidiwa na mfuko wa mazingira duniani, (GEF) kuwezesha upatikanaji wa takwimu kuhusu misitu, zilizo za uwazi na haswa zinazosaidia nchi zinazoendelea kutekeleza makubaliano ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Ufuatiliaji na utoaji taarifa kuhusu misitu na matumizi ya ardhi ni muhimu katika ufuatiliaji na utekelezwaji wa maendeleo endelevu. Mradi huo unafadhiliwa na GEF kwa dola milioni 1.9 na pia FAO ambayo inachangia dola milioni 5.2, ni mmoja kati ya miradi minne tu duniani iliyoidhinishwa na kufadhiliwa na mfuko  mpya unaosaidia nchi kutekeleza mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

“Nchi nyingi zinazoendelea hukosa uwezo wa kutoa takwimu muhimu kuhusu misitu ili kuripoti mafanikio yao kuhusu tabianchi. Mradi huu utasaidia kuwepo mfumo wa kutegemewa na uwazi katika takwimu za misitu na kusaidia nchi kukusanya na kujumuisha data kuambatana na makubaliano ya Paris”, amesema Hiroto Mitsugi, Naibu Mkurugenzi wa FAO idara ya misitu.

Mradi huo utanufaisha moja kwa moja nchi 26 kote barani Asia, Afrika na Amerika Kusini na nchi zingine 185 kote duniani.

Utatekelezwa katika kipindi cha miaka miwili na idara ya msitu ya FAO ambayo tayari inasaidia nchi 70  kufuatilia misitu, kuhakikisha usimamizi bora wa misitu na utoaji wa ripoti za misitu zilizo bora.