Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano mapya kuhusu uhamiaji ni suluhu ya masuala mengi- Espinosa

María Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani
UN /Manuel Elias
María Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani

Makubaliano mapya kuhusu uhamiaji ni suluhu ya masuala mengi- Espinosa

Wahamiaji na Wakimbizi

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa María Fernanda Espinosa, amesema anaelewa fika uamuzi wa baadhi ya mataifa wa kutokuwa tayari kutia saini makubaliano mapya kuhusu uhamiaji baadaye mwaka huu.

Bi. Espinosa amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani,  mkutano ambao umefanyika ili kutoa ripoti ya kile alichofanya tangu baada ya kumalizika kwa mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza analoongoza.

Amesema baadhi ya nchi zinataka majadiliano na mashauriano zaidi ndani ya nchi ambapo amesema “uzuri wa mkataba huu ni kwamba unatoa fursa kwa nchi kuangalia kile ambacho inaweza kuchukua na kujumuisha kwenye maamuzi yake ya ndani, kama vile mifumo ya kisheria. Na ni muundo, ni ushirikiano na ni mbinu ya kufanyia kazi.”

Ameelezea kuwa makubaliano hayo ni ya kihistoria ambayo yatasaidia kuhakikisha kuwa wahamiaji kila mahali duniani haki zao zinalindwa na wanatendewa kwa haki.

UNNewsKiswahili/Assumpta Massoi
Uhamiaji!

Mkataba huo unatarajiwa kutiwa saini huko Marrakesh, Morocco mwezi ujao wa Disemba na unaweka malengo mahsusi ya kuhakikisha uhamiaji unakuwa salama, unafuata kanuni na unakuwa wa kawaida, ukishughulikia shaka na shuku za serikali na kuimarisha mamlaka za kitaifa bila kusahau kutambua hatari wanazokumbana nazo wahamiaji.

Bi. Espinosa amesema anatiwa moyo na ari ya nchi wanachama na anatarajia kuwa mkutano huo utakuwa wa mafanikio makubwa akisema kuwa, “uhamiaji ni njia ya kuendeleza dunia, unaunganisha watu. Na hivi karibuni hata hivyo tumeshuhudia mwelekeo usio wa kawaida wa uhamiaji ambao unapaswa kushughulikiwa kimataifa na jibu ni mkataba wa kimataifa wa uhamiaji.

Kauli hiyo ya rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imekuja wakati mataifa kadhaa yakiripotiwa kutangaza kuwa hayatounga mkono makubaliano  hayo, na nchi hizo ni pamoja na Israel, Marekani na Australia.