Sasa mkataba wa Marrakech ni rasmi, Baraza Kuu la UN laupitisha

19 Disemba 2018

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limepitisha kwa kishindo mkataba wa kimataifa wa uhamiaji salama, wenye mpangilio na unaofuata kanuni za kawaida.

Wawakilishi wa nchi wanachama wamepiga kura katika kikao mahsusi cha kupitisha azimio hilo ambapo kura 152 ziliunga mkono, kura 5 zilipinga ilhali nchi 12 hazikupigia kabisa kura azimio hilo ambapo linajulikana pia kama mkataba wa Marrakech.

Nchi ambazo zimepiga kura ya hapana ni Jamhuri ya Czech, Hungary, Israel, Poland na Marekani.

Mkataba huo ulipitishwa wiki iliyopita huko Marrakech nchini Morocco baada ya mashauriano yaliyohusisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kufuatia hatua ya Baraza hilo Kuu kupitisha mkataba huo, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema  nyaraka hiyo ambayo licha ya kwamba haina shuruti ya kisheria, inapatia msisitozo misingi ya jamii ya kimataifa ikiwemo mamlaka ya kitaifa, haki za binadamu huku ikitoa maelekezo juu ya hatua bora kwa wahamiaji kwa maslahi ya nchi wanazotoka, wanakoenda na pia kwa maslahi yenye utu ya wahamiaji wenyewe.

“Katika wakati ambao ushirikiano wa kimataifa ni muhimu kuliko wakati wowote, mkataba mpya wa kimataifa wa uhamiaji unaweka jukwaa muhimu kwa ushirikiano huo,” amesema Guterres akishukuru pande zote zilizofanikisha hatua hiyo akiwemo Rais wa sasa wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa na mtangulizi wake Miroslav Lajčák.

Mapema akizungumza kabla ya  kupitishwa kwa azimio hilo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bi. Espinosa alieleza wajumbe kuwa mkataba huo wa Marrakech ni taswira ya utashi wa mataifa kushughulikia kwa pamoja na kwa njia sawia changamoto kubwa ya sasa ya uhamiaji.

Amesema ni fursa ya kihistoria “ya ushirikiano, kubadilishana mbinu bora za kupatia suluhu suala hilo na pia kujifunza kutoka kila upande ili uhamiaji uwe na maslahi kwa kila mtu.”

Wakati huo huo, mtandao wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji, ambayo unajumuisha taasisi, ofisi na mashirika 33 ya umoja huo, umetoa taarifa ukisema, “kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa wa uhamiaji na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni tukio la kipekee katika kusaka ushirikiano wa kimataifa na kuwa na uhamiaji unaonufaisha kila sisi sote.”

Louise Arbour ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji wa kimataifa, amesema hatua hiyo inaashiria kukubaliwa kwa mfumo huo wa kimataifa unaozingatia taarifa sahihi badala ya fikra potofu na kuelewa kuwa sera bora za kitaifa zinatekelezwa vyema kupitia ushirikiano wa kimataifa na si kwa kujitenga.

UN /Manuel Elias
Matokeo ya upigiaji kura mkataba wa Marrakech kwenye Baraza Kuu la UN jijini New York, Marekani leo Desemba 19, 2018.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Umoja wa Mataifa wapitisha rasmi mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi

Mamilioni ya watu kote duniani hutumia miaka mingi ya maisha yao ukimbizini na wengine wakihatarisha maisha yao katika harakati za kusaka usalama wakienda wasikokujua. Amesema hayo leo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi Amina J. Mohammed, wakati wa hafla ya kupitisha rasmi mkataba mpya wa wakimbizi, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani. 

FAHAMU: Mkataba wa kimataifa wa wakimbizi na mkataba wa kimataifa wa uhamiaji salama

Mkataba wa kimataifa wa wakimbizi: Tofauti ni ipi na mkataba wa wahamiaji na ni kwa vipi utasaidia watu waliolazimika kukimbia makwao?