Njia ya kupitisha mkataba mpya wa wahamiaji sasa ni ‘nyeupe’- UNHCR

13 Novemba 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema sasa kuna matumaini makubwa ya kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbiz na wahamiaji, GCM mwezi ujao.

Tamko hilo la UNHCR linazingatia kitendo cha kamati ya tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya kijamii, kibinadamu na kitamaduni, kupitisha kwa kishindo azimio kuhusu kazi za shirika hilo lenye jukumu la kusimamia wakimbizi duniani.

Kinachosubiriwa hivi sasa ni Baraza Kuu kupitisha azimio hilo baadaye mwaka huu ambapo UNHCR inasema kuwa mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi unapaswa kupitishwa kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2018.

“Azimio la leo ni kiashiria muhimu kwa uungaji mkono wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi na kazi za UNHCR. Mkataba huo uliandaliwa baada ya kazi nzito ya miezi 24 ikijumuisha mijadala na nchi wanachama, wataalamu, mashirika ya kiraia na wakimbizi na mpango wa matumizi yake uliwekwa bayana ya azimio la New York kuhusu wakimbizi na wahamiaji tarehe 19 mwezi Septemba mwaka 2016,” imesema taarifa ya UNHCR.

Mkataba huo unapigia chepuo hatua bora, thabiti na sahihi kuhusu ushughulikiaji wa mienendo ya wakimbizi duniani.

Malengo makuu ni pamoja na kupunguza shinikizo kwa nchi ambazo zinahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi na kusaidia wakimbizi wajitegemee.

Ni kwa mantiki hiyo UNHCR imetoa shukrani za dhati kwa nchi wanachama ikiitaja zaidi Sweden ambayo ilizingatia kwa kina zaidi azimio hilo.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter