TV bado haijapoteza dira licha ya teknolojia mpya:UN

21 Novemba 2018

Televisheni bado ni chombo muhimu cha mawasiliano duniani licha ya kuzuka kwa teknolojia mpya ambazo zimechukua nafasi kubwa ya maisha ya watu, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni, UNESCO. 

Katika kuadhimisha siku ya televisheni duniani ambayo kila mwaka huwa Novemba 21, UNESCO inasema kama ilivyo kwa Radio, bado sehemu kubwa ya jamii  inategemea kuangalia televisheni kwa ajili ya kupata taarifa, kuhafamu yanayojiri kwingineko duniani, kuelimika na kufuatilia matukio mbalimbali.

UNESCO inasema tekinolojia kama komputa mpakato, Ipadi na simu za kiganjani au za rununu vimechukua sehemu kubwa ya maisha ya watu hivi sasa. Kwa mfano takwimu zinaonyesha kwamba watu wanatumia muda mwingi kwenye simu za kiganjani au za rununu kuliko jumla ya watu wote wanaosoma magazeti na kusikiliza Radio duniani.

Kwa Umoja wa Mataifa tangu kuanzishwa kwa UN TV mwaka 1947 imechangia kwa kiasi kikubwa kufikisha ujumbe wa kazi na umuhimu wa Umoja huo duniani kote katika masuala kama amani na usalama, haki za binadamu, maendeleo, masuala ya watu wenye ulemavu, ulinzi wa amani, wakimbizi na wahamiaji na pia mabadiliko ya tabia nchi.

Televisheni chombo kilichozinduliwa miaka ya 1920, kinasalia kuwa ni chanzo kikubwa cha watu kutazama video duniani huku idadi ya nyumba zilizo na televisheni zikitarajiwa kuongezeka duniani kutoka bilioni 1.63 mwaka 2017 hadi bilioni 1.74 mwaka 2023

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter