Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

‘Reggae’ ya Jamaica na tambiko la kijapani vyatambuliwa na UNESCO

Mtindo wa muziki wa Reggae kutoka Jamaica umejumuishwa kwenye orodha ya turathi za kitamaduni zisizogusika.
Semiyah Photography, 2017
Mtindo wa muziki wa Reggae kutoka Jamaica umejumuishwa kwenye orodha ya turathi za kitamaduni zisizogusika.

‘Reggae’ ya Jamaica na tambiko la kijapani vyatambuliwa na UNESCO

Utamaduni na Elimu

Mtindo wa muziki wa ‘reggae’ kutoka Jamaica, mieleka ya Georgia na matambiko ya kijapani ni miongoni mwa tamaduni ambazo hii leo zimejumuishwa katika orodha ya turathi za tamaduni zisizogusika za kibinadamu za shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO.

Hatua hiyo imefikiwa huko Port Louis, mji mkuu wa Mauritius ambako kamati ya kiserikali ya UNESCO ya kulinda turathi za tamaduni zisizogusika inakutana hadi tarehe mosi mwezi ujao kuangazia tamaduni mbalimbali zenye  hadhi ya kujumuishwa kwenye orodha.
 
Taarifa ya UNESCO ikichambua tamaduni hizo zilizojumuishwa leo kwenye orodha, imetolea mfano mtindo wa muziki wa ‘reggae’ kutoka Jamaica ikisema kuwa umeasisiwa kutoka tamaduni za makundi yaliyo pembezoni hususan magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Kingston. 
 
“Mtindo huo wa muziki kutoka Jamaica unaunganisha mahadhi kutoka Jamaica ya asili pamoja na Karibea, Amerika ya Kaskazini na Amerika ya Kusini. Jukumu lake kuu la kusongesha mjadala wa kijamii kama uzoefu usio na muingilio, ukimsifu Mungu, haujabadilika na muziki unaendelea kutoa fursa ya kupaza sauti kwa wote,” imesema taarifa ya UNESCO.
 
Imeongeza kuwa wanafunzi wanaendelea kufundishwa jinsi ya kucheza mtindo huo tangu wakiwa watoto na katika matamasha na majukwaa mbalimbali ili kuhakikisha mwendelezo wake.
 
Kwa upande wake matambiko ya kijapani ni yale yaliyopatiwa jina la Raiho-shin na kutembelea mahekalu waumini wakiwa wamevaa vinyago.
 
“Matambiko ya Raiho-shin hufanyika kila mwaka katika sehemu mbalimbali nchini Japan katika siku za kusherehekea mwaka mpya au kubadilika kwa msimu,” imesema ripoti hiyo ikifafanua kuwa “matambiko haya yanatokana na imani za kale ya kwamba Mungu wao huyo au Raiho-shin, atatembelea jamii na kuwaashiria kuanza kwa mwaka mpya au msimu mpya.”
 
UNESCO imesema upekee wa tamaduni hii ni kwamba wakati wa tambiko, wakazi wa eneo husika huvalia mavazi ya kipekee na ya kuvutia wakitembelea nyumba huku wakionya watu waache uzembe na kufundisha watoto tabia njema. 
 
“Baada ya hapo, mkuu wa familia iliyotembelewa na Raiho-shin anawapatia Mungu hao mlo maalum ijapokuwa baadhi ya jamii tambiko hilo hufanyika mitaani,” imesema UNESCO.