Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Redio bado ni chombo chenye nguvu-Antonio Guterres

Lydie Mpambara (kushoto) wa Idara ya Baraza Kuu na mikutano ya Umoja wa Mataifa akihojiwa na Anold Kayanda wa UN News Kiswahili
UN News/Assumpta Massoi
Lydie Mpambara (kushoto) wa Idara ya Baraza Kuu na mikutano ya Umoja wa Mataifa akihojiwa na Anold Kayanda wa UN News Kiswahili

Redio bado ni chombo chenye nguvu-Antonio Guterres

Utamaduni na Elimu

Jumatano hii, kama ilivyo ada kila mwaka Februari 13, dunia inaadhimisha siku ya redio duniani ujumbe ukiwa majadiliano, uvumilivu na amani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake kwa ulimwengu kuhusu siku hii amesema redio ni chombo chenye nguvu. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hata katika dunia ya sasa ya mawasiliano ya kidijitali, redio inawafikia watu wengi zaidi ya chombo kingine chochote cha habari.

Akisisitiza hoja zake, Bwana Guterres amesema,“Inafikisha taarifa muhimu na kuelimisha kuhusu masuala muhimu na kuwa ni chombo kinachozungumza na muhusika moja kwa moja na kumshirikisha na watu wanaweza kutoa maoni yao, kueleza wasiwasi wao na malalamiko yao pia redio inaweza kujenga jamii”

Kwa Umoja wa Mataifa, hususan kwa operesheni  za ulinzi wa amani Guterres amesema, “Redio ni njia muhimu ya kufikisha taarifa, kuunganisha na kuwawezesha watu walioathirika na vita. Katika siku hii ya redio duniani, hebu tutambue uwezo wa redio katika kuchagiza majadiliano, uvumilivu na amani”

Maadhimisho ya siku ya redio duniani tarehe 13 Februari yanatokana na siku ambayo redio ya Umoja wa Mataifa ilianzishwa kmwakaa 1946.