Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uholanzi ondoeni ubaguzi wa rangi katika mfumo wa ustawi wa jamii: UN

Watoto wakiwa nje ya madarasa yao wakicheza sehemu za Curaçao, Uholanzi.
Photo: UNICEF/Roger LeMoyne
Watoto wakiwa nje ya madarasa yao wakicheza sehemu za Curaçao, Uholanzi.

Uholanzi ondoeni ubaguzi wa rangi katika mfumo wa ustawi wa jamii: UN

Haki za binadamu

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi mkubwa juu ya ubaguzi wa rangi katika mfumo wa ustawi nchini Uholanzi, wakitumia mfano wa tukio la familia moja ya wakimbizi wenye asili ya Afrika wanaoishi nchini  humo ambayo ilinyang’anywa usimamizi wa watoto wao.

Kitendo hicho kimefanyika wakati utafiti unaonyesha kwamba kuna mitazamo hasi dhidi ya wazazi wa asili ya kiafrika, wamesema wataalam hao wa Umoja wa Mataifa na kwambab kuna tofauti jinsi mfumo wa ustawi wa jamii unatendea familia za watu weupe wa Uholanzi ikilinganishwa na wale wa asili ya Afrika.

Katika tukio hilo, inaelezwa kuwa mwezi Mei mwaka huu, polisi waliwachukua watoto saba akiwemo mtoto mchanga anayenyonya bila kuzingatia maslahi ya watoto au muundo wa familia au hata kwanza kutoa mafunzo ya namna ya kutatua matatizo katika familia.

“Uamuzi wa kuwachukua watoto katika familia zao ulichukuliwa hata pasipo usimamizi wa mahakama na katika miezi mitatu tangu watoto walipotenganishwa na familia zao, wazazi  hawajaruhusiwa kuwatembelea watoto na watoto hawajaweza kuwaona wazazi wao,” wamesema wataalamu hao.

“Kutenganishwa kwa familia kumesababisha matatizo ya kiakili na kisaikolojia na tuna wasiwasi juu ya  athari kwa ustawi wa kimwili na kiakili wa watoto. Kutenganisha kokote kwa mtoto na wazazi wake kunatakiwa kuwa jambo la mwisho na kunapaswa kuzingatia sheria za kimataifa za haki za binadamu. Tumeieleza serikali ya Uholanzi kuhusu wasiwasi wetu, na tumewaomba kuchunguza kuchunguza tukio hilo, kuunganisha familia na kuhakikisha haki sawa mbele ya sheria ” wamesema wataalamu.

Taarifa ya wataalam imeeleza kuwa serikali ilikanusha madai ya ukandamizaji kwa misingi ya rangi na ikadai ubaguzi wa rangi unaweza kuripotiwa polisi au katika vitengo vya kupambana na ubaguzi.

Wataalam hao wa Umoja wa Mataifa wameitaka serikali ya Uholanzi ihakikishe kunakuwepo na nafasi kwa familia zilizotenganishwa kutembeleana mpaka watakapounganishwa tena na ichukue hatua za kumaliza ubaguzi kwa misingi ya rangi katika mfumo wa ustawi wa watoto.