Tumepiga hatua lakini bado tuna kazi katika kutimiza haki za mtoto:Guterres

Mtoto wa kike nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa akiwa ameshika kibao chenye sehemu ya mkataba wa haki za watoto CRC.
UNICEF
Mtoto wa kike nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa akiwa ameshika kibao chenye sehemu ya mkataba wa haki za watoto CRC.

Tumepiga hatua lakini bado tuna kazi katika kutimiza haki za mtoto:Guterres

Haki za binadamu

Tangu kupitishwa kwa mkataba wa haki za mtoto miaka 30 iliyopita pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kote duniani bado vita imesalia kuwa chanzo kubwa ya ukiukwaji wa haki za mtoto na bado kuna nchi hazijaridhia mkataba huo amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. 

Katibu Mkuu akizungumza katika hafla hiyo leo jijini New York Marekani kandoni mwa mjadala Mkuu wa Baraza kuu , amesema “mkataba huo unatambua kwamba mtoto ana haki ya kulindwa na kuwa na uhakika wa usalama wao majumbani, wanakoishi na vijijini kwao, wana haki ya kutoa maoni yao na kusikilizwa na mkataba huu ni moja ya mikataba ya Umoja wa Mataifa iliyoridhiwa na nchi nyingi sana katika historia. Lakini bado kuna baadhi ya nchi wanachama ambao bado hawajafanya hivyo na matarajio ni kufikia siku ambayo wajumbe wote wataunga mkono mkataba huu."

Hata hivyo amesema, “kuchukua au kutochukua hatua kwa serikali kuna athari kubwa kwa watoto kuliko kundi lingine lolote katika jamii, watoto wako katika hatari ya umasikini, njaa, afya duni na maisha wasiyostahili. Lakini kwa juhudi zilizofanyika haki sasa imedhihirika kwa mamilioni ya watoto. Lakini hatuwezi kumudu kubweteka , tunahitaji kuimarisha juhudi zetu kuhakikisha kwamba watoto wote wako salama, wana afya na wanaweza kutimiza ndoto zao.”

Naye binti mdogo kutoka Ghana aliyeiwakilisha nchi yake na watoto wote wa Afrika amesisitiza, “ndio tumepiga hatua lakini bado kuna mengi ya kufanya kwa watoto wanaoishi katika umasikini na kutelekezwa, kwa watoto wanaoishi katika vita, ukimbizi na jamii za wahamiaji."