Wahisani watoa dola milioni 38 kunusuru meli iliyo hatarini kupasuka baharí ya Sham karibu na Yemen

11 Mei 2022

Takribani dola milioni 38 zimechangishwa ili kunusuru meli ya kuhifadhi mafuta, FSO Safer iliyo hatarini kuzama na kuvujisha mafuta au kulipuka kando mwa pwani ya Yemen. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP nchini Yemen, limesema hayo kupitia mtandao wake wa Twitter hii leo baada ya mkutano uliofanyika The Hague, Uholanzi kuchangisha fedha za kunusuru meli hiyo iliyoanza kuoza kwa kuweko baharini muda mrefu bila kukarabatiwa na bila kufanya shughuli zozote. 

 

Safer ni nini? 

Safer ndio meli hiyo ambayo ilitengenezwa mwaka 1976 kwa ajili ya kubeba na kusafirisha mafuta lakini muongo mmoja baadaye iligeuzwa na kufungwa mnyororo huku ikielea baharí kwa ajili ya  kuhifadhi mafuta. 

Imefungwa mnyororo umbali wa maili za baharini 4.8 kutoka pwani ya jimbo la Hudaydah nchini Yemen ikiwa na mapipa milioni 1.14 ya mafuta ghafi. 

Kazi ya kuzalisha, kushusha mafuta na kuikarabati ilisitishwa mwaka 2015 kutokana na vita nchini Yemen na sasa hali yake inazidi kudorora. 

Tathmini inaonesha kuwa kwa sasa haiwezi tena kukarabatiwa na iko hatarini mafuta kuanza kuvuja au meli kulipuka kwa sababu mifumo ya kuingiza gesi kwenye tanki za mafuta ili kuepusha vitendo hivyo ilikufa mwaka 2017. 

Yemen haina uwezo wa kukabili madhara yatokanayo na kuvuja au kulipuka kwa meli hiyo. 

Gharama husika 

Gharama ya usafishaji iwapo mafuta yatavuja ni dola bilioni 20, fedha zinazosakwa zinalenga kutekeleza mpango wa kunusuru unaogharimu dola milioni 79.6 ambapo kati ya hizo dola milioni 35 ni kwa ajili ya kuiweka katika mazingira isizidi kuharibika zaidi na kukodisha meli nyingine ya kubeba mafuta kushikilia mafuta hayo kwa miezi 18, bima, wafanyakazi na kadhalika. 

UN imefanya nini? 

Guterres anasema mpango wa Umoja wa Mataifa unaweza kuepusha janga kwa SAFER kabla halijatokea. 

Miezi ya karibuni Umoja wa Mataifa ulishirikiana na wadau kusaka njia ya kutatua, mpango uliungwa mkono na sasa fedha zinahitajika. 

“Tukio la leo ni hatua muhimu ya kuzuia janga ambalo litaathiri Yemen, Kanda na dunia nzima,” amesema Katibu Mkuu huku akisihi wadau wa Yemen watoa fedha ili kazi ianze mara moja. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter