Majanga yanavyozidi kushamiri isiwe kisingizio cha kusigina haki za mtoto- UN

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa hususan zile za mtoto wametoa taarifa ya pamoja hii leo huko Geneva, Uswisi wakisema majanga ya kiafya, kibinadamu na yale yanayohusiana na tabianchi yakizidi kuongeza changamoto kubwa duniani kila uchao kama vile ukimbizi wa ndani, ukatili wa kingono na njaa, serikali lazima zikumbuke kuwa watoto wana haki kamilifu za kimsingi za kibinadamu na kwamba haki hizo zinapaswa kulindwa.
Taarifa iliyotolewa leo New York, Marekani na Geneva Uswisi imetaja wataalamu hao kuwa ni wale wa kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za mtoto, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kwenye mizozo ya kivita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu ukatili dhidi ya watoto , UNICEF na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabili uhalifu na madawa ya kulevya.
Wamesema nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa lazima watambue kuwa watu wote wenye umri wa chini ya miaka 18 ni watoto wana haki mahsusi kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa haki za mtoto, CRC, ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa.
Tunashuhudia ongezeko la kushindwa kuzingatia wajibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na za kibinadamu wamesema wataalamu hao wakiongeza kuwa watoto na familia zao wanaendelea kukimbia makazi yao huku mizozo nah atua za serikali za kukabili vikundi vilivyojihami zikichangia zaidi katika mmomonyoko wa wa mifumo ya kimataifa ya ulinzi, na mara nyingi ukiukaji wa haki za mtoto.
Wamekumbusha serikali kuwa mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC ambao umeridhiwa na mataifa 196 unapaswa kuzingatiwa na kulinda haki za watu wote wenye umri wa chini ya miaka 18.
“Tunasisitiza kuwa nchi wanachama zina wajibu wa kulinda, kuheshimu na kutekeleza haki za mtoto iwe wakati wa vita au wakati wa amani bila kujali umri, jinsia, hadhi, nchi anakoishi, au anakotoka. Watoto wote wanastahili kupatiwa haki zao ikiwemo ya kuishi, kuendeleza, kufurahia afya bora ikiwemo ya akili, elimu, kucheza na kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote,” wamefafanua wataalamu hao.
Kwa sasa wanasema haki hizo za watoto zinasiginwa ikiwemo kwa watoto wanaoishi kwenye maeneo ya mizozo au mazingira ambamo vita imemalizika.
Hofu yao kubwa zaidi pia ni mazingira ambamo kwamo watoto wenye umri fulani kuchukuliwa kuwa ni watu wazima au vijana. Katika baadhi ya matukio hii inakuwa ni kwa kisingizio cha mila na utamaduni au harakati za kukabili ugaidi na hivyo kuwazuia haki yao ya msingi ya kufurahia haki zao kwa mujibu wa CRC.
Pamoja na kusisitiza umuhimu wa nchi zilizosalia kusaini na kuridhia mkataba huo kufanya hiyo, wataalamu hao wamekumbusha kuwa utoto ni awamu muhimu nay a kipekee katika maisha ya binadamu ambapo watoto wana haki maalum zinazotambuliwa na CRC. Tunatoa wito kwa serikali izingatie wajibu wao kwa mujibu wa mkataba huo.