Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa lazinduliwa kukabili tishio la usugu wa dawa dhidi ya binadamu na wanyama

Daktari akichambua sampuli katika maabara ya vijiumbe maradhi kwenye hospitali ya mafunzo ya Chuo Kikuu cha Obafemi Awolowo nchini Nigeria
© WHO/Etinosa Yvonne
Daktari akichambua sampuli katika maabara ya vijiumbe maradhi kwenye hospitali ya mafunzo ya Chuo Kikuu cha Obafemi Awolowo nchini Nigeria

Jukwaa lazinduliwa kukabili tishio la usugu wa dawa dhidi ya binadamu na wanyama

Afya

Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa leo yamezindua jukwaa jipya la ubia wa pamoja katika kukabiliana na usugu wa viua vijiumbemaradhi ambao unatishia afya ya binadamu, wanyama na mfumo wa ikolojia duniani kote na hivyo kusaka hatua za pamoja,

Taarifa iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, limetaja mashirika hayo kuwa ni lenyewe WHO, lile la chakula na kilimo, FAO, la mazingira UNEP na la afya ya wanyama, WOAH.

Takribani watu milioni 1.3 duniani kote wanakufa kila mwaka kutokana na usugu wa viua vijiumbe maradhi, AMR.

Iwapo hatua hazitochukuliwa, idadi hiyo inaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa na kuongeza gharama ya afya ya umma na kuzidi kutumbukiza watu wengi zaidi kwenye lindi la umaskini hasa kwenye nchi za kipato cha chini na hivyo jukwaa litahamasisha juhudi za pamoja,” imesema taarifa hiyo.

Dawa aina ya viuavijasumu au antibiotics na aina nyingine za dawa za kuua vijiumbe maradhi au antimicrobials zina dhima muhimu katika mafanikio ya matibabu ya kisasa na zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha afya ya binadamu na wanyana.

“Hata hivvoy matumizi kupita kiasi au matumizi holela ya dawa hizo yamepunguza ufanisi wake, ambapo sasa vijidudu vingi zaidi vinajijengea usugu wa kuendelea kuishi na dawa hizo viua vijiumbemaradhi zilizotengenezwa kuvikabili zinazishindwa kuvitokomeza,” imesema taarifa hiyo.

Usugu wa viua vijiumbemaradhi huanza vipi?

Usugu wa viua vijiumbe maradhi au hutokea pale vimelea, bakteria, virusi na fangasi vinashindwa kutokomezwa na viua vijiumbe maradhi. Na kutokana na usugu huo wa dawa, viuavijasumu, viua vijiumbe maradhi vinakuwa havina ufanisi na hivyo inakuwa vigumu kutibu maambukizi na hatimaye magonjwa kusambaa, ugonjwa unakuwa mkali na kisha kifo.

Halikadhalika, zaidi ya watu bilioni 1.3 wanategemea mifugo kama njia yao ya kujipatia kipato na watu milioni 20 wanategemea ufugaji samaki, hasa katika nchi za kipato cha chini na kati.

Mazingira safi katika maeneo ya mifugo inaweza kupunguza matumizi ya viuavijasumu
FAO/Sergei Gapon
Mazingira safi katika maeneo ya mifugo inaweza kupunguza matumizi ya viuavijasumu

Usugu wa dawa na athari kwenye kipato

“Kusambaa kwa usugu wa dawa unaathiri mbinu za watu kujipatia kipato, ongezeko la magonjwa ya wanyama na vifo. Matumizi ya dawa hizo kwenye mazao pamoja na utupaji holela wa dawa zilizopita muda wake au ambazo hazijatumika, kutoka viwandani au kwneye jamii, kunaweza pia kusababisha uchafuzi wa udongo na mito na kuchochea kusambaa kwa vijidudu kunakoweza kuleta usugu na hivyo kushinwa kutibika,” imesema taarifa hiyo.

Wakuu wa WHO, FAO, UNEP na WOAH wapaza sauti

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema usugu wa viua vijiumbe maradhi unatishi afya ya wanyama, usalama wa chakula, uhakika wa kupata chakula, ustawi wa kiuchumi na wa kiikolojia duniani kote, “dunia inahitaji kuunganisha juhudi sasa ili kuzuia usugu wa dawa kwa magonjwa na kupunguza athari zake.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen amesema changamoto dhidi ya AMR haziwezi kutambuliwa kwa kushughulikia kitofauti tofauti badala yake juhudi za pamoja ndio jawabu hasa wakati huu ambapo tabianchi nayo imeshika kasi kuleta madhara.

Kwa Dkt Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, jukwa lisaidia kuchagiza uratibu wa kimataifa ili hatua za pamoja ziwe za kimkakati zaidi, rasilimali zitumike kwa ufanisi na ziwe endelevu.

Monique Eloit, Mkurungezi Mkuu wa WOAH amesema “tunaweza kuchukua hatua mapema dhidi ya AMR tukiwa na ubia huu sahihi na miundo ya ushirikiano. Wakati wa kuchukua hatua ni sasa. Tunahaha kulinda kila mtu dhidi ya tishio la usugu wa viua vijiumbemaradhi.”

Uzinduzi wa jukwaa hili umefanyika leo ambayo ni siku ya kuanza kwa Wiki ya uhamasishaji kuhusu vijiumbe maradhi.