Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji vijijini ni muarobaini wa amani ya kudumu duniani- IFAD

Mbinu kama hizi za kusafirisha mazao kupeleka sokoni hazina tija kwa mkulima.
©FAO/Pius Utomi Ekpei
Mbinu kama hizi za kusafirisha mazao kupeleka sokoni hazina tija kwa mkulima.

Uwekezaji vijijini ni muarobaini wa amani ya kudumu duniani- IFAD

Amani na Usalama

Kuelekea jukwaa la amani litakaloanza kesho huko Paris, Ufaransa, Rais wa mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD Gilbert F. Houngbo, amesema atatumia kusanyiko  hilo kuwaeleza viongozi wa dunia juu ya umuhimu wa kuwekeza vijijini.

Bwana Hungbo amenukuliwa kupitia taarifa ya IFAD iliyotolewa Roma, Italia akisema kuwa “kuongeza uwekezaji vijijini ni suluhisho la kumaliza visababishi vya mizozo duniani,” na kwamba amani na utulivu haviwezekani pindi watu wanapokuwa na njaa, maskini au wanaenguliwa kwenye harakati za maendeleo.

Mkuu huyo wa IFAD amesema kiwango cha ukosefu wa chakula duniani kikiongezeka kwa mwaka wa tatu mfululizo, “sasa kuna udharura wa kuongeza uwekezaji kwa maendeleo ya muda mrefu ambayo yataleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii maeneo ya vijijini.”

Bwana Houngbo amesema njaa na umaskini ni madhila ya dunia ambayo yanaweza kupatiwa suluhu kupitia harakati za pamoja zinazohusisha serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na taasisi za kimataifa pamoja na taasisi za utafiti, wasomi na zaidi ya yote wanawake na wanaume wa vijijini.

Takribani asilimia 80 ya watu maskini zaidi na wasio na uhakika wa chakula wanaishi maeneo ya vijijini, imesema IFAD ikiongeza kuwa uhakika wa chakula ni moja ya misingi ya kuwepo kwa jamii zenye amani ikinukuu azimio la Umoja wa Mataifa namba 2417 lililopitishwa mwezi Mei mwaka jana.

Mkutano huo wa siku mbili  utaanza kesho na utaleta pamoja zaidi ya viongozi 60 wa nchi pamoja na wale wa  mashirika ya kiraia kwa lengo la kujadili utawala bora duniani na hatua thabiti za kujenga amani ya kudumu duniani.