Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

SOFI 2018 yaonesha pande mbili za uhakika wa chakula duniani

Hali ya uhakika wa chakula
Source: Global Report on Food Crises
Hali ya uhakika wa chakula

SOFI 2018 yaonesha pande mbili za uhakika wa chakula duniani

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Baada ya maendeleo ya muda katika masuala ya uhakika wa chakula na lishe duniani, ushahidi unaonesha kuwa njaa inaendelea kuongezeka,  imesema ripoti ya mwaka huu ya hali ya uhakika wa chakula na lishe duniani, SOFI, iliyochapishwa hii leo. Taarifa zaidi na Arnold Kayanda.

Ikiwa imeandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la chakula na kilimo FAO, mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo IFAD, la kuhudumia watoto, UNICEF, la afya WHO na mpango wa chakula, WFP, ripoti inaonesha kuwa idadi ya watu ambao wanakabiliwa na njaa imeongezeka kwa miaka mitatu mfululizo kutoka milioni 804 mwaka 2016 hadi milioni 821 mwaka jana.

Bara la Afrika linasalia kuwa lenye kiwango cha juu cha watu wasiopata lishe bora ya kutosha, hali inayoathiri asilimia 21 ya watu wote yaani zaidi ya watu milioni 256 barani humo.

 Hali pia inadorora katika Amerika ya kusini ambapo wasiopata mlo bora wameongezeka kwa asilimia 4.7 kwa mwaka 2014 mpaka asilimia 5.0 kwa mwaka 2017.

Migogoro, mabadiliko ya tabia nchi na mdororo mkubwa wa uchumi ni vichocheo vya kuongezeka kwa njaa duniani.

Ripoti inasema hata katika nchi au mazingira ambayo hayajaathiriwa na migogoro, mabadiliko ya tabia nchi au anguko la uchumi, ufukara na kuenguliwa kwa jamii kumesababisha baadhi ya watu wasipate lishe bora.

SOFI pia imeongeza kuwa kama ilivyo hali ya kutisha ya kuongezeka kwa njaa, utapiamlo nao unashuhudiwa huku utipwatipwa nao ukiongezeka katika maeneo yote ya dunia pia ukiathiri nchi zinazoendelea katika upande wa afya, maisha na uchumi.

Hata hivyo ripoti imeeleza kuwa, kiujumla kumekuwa na maendeleo katika suala la watoto kunyonya katika kipindi cha miezi sita ya maisha yao  na kupungua kwa watoto wanaodumaa na wanaoongezeka kwa .

Idadi ya watoto wanaodumaa imeshuka kwa asilimia 9 kutoka milioni 165.2 kwa mwaka 2012 hadi milioni 150 kwa mwaka 2017, japokuwa si idadi inayokubalika bado na hilo linafanya lengo la mwaka 2030 kuwa mbali sana kufikiwa.