Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC ni mshumaa uliowashwa miaka 20, tusiache uzimike- Jaji Eboe-Osuji

Jaji Chile Eboe-Osuji, Rais wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC akiwasilisha ripoti ya mwaka ya utendaji ya chombo hicho mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN /Loey Felipe
Jaji Chile Eboe-Osuji, Rais wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC akiwasilisha ripoti ya mwaka ya utendaji ya chombo hicho mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

ICC ni mshumaa uliowashwa miaka 20, tusiache uzimike- Jaji Eboe-Osuji

Masuala ya UM

Rais wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC Jaji  Chile Eboe-Osuji amesema ushirikiano wa kimataifa ndio nguzo pekee ya kuendeleza kazi za mahakama hiyo iliyoanzishwa miaka 20 iliyopita.

Akihutubia baraza hilo leo wakati wa kuwasilisha ripoti ya utendaji ya ICC kwa mwaka 2017/2018 Jaji Eboe-Osuji amesema ushirikiano  huo ni muhimu kwa kuwa chombo hicho kinatahijika zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule.

Amesema vitendo vya ukatili vimeshamiri, uhalifu wa kivita unaripotiwa huku na kule akirejelea mauaji ya kimbari Rwanda na yale ya halaiki huko Srebrenica akisema, "ICC ni chombo halisi tulicho nacho hivi sasa kwa ajili ya kuhukumu wale ambao watatenda uhalifu kama huo, kwa lengo la kuepusha usitokee tena siku za usoni. Nawasihi mfanya ICC iwe thabiti kila siku. Katu msikuhali iwe dhaifu.”

Rais huyo wa ICC ambaye ni mara ya kwanza kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa  Mataifa tangu achaguliwe kushika wadhifa huo mwezi Machi mwaka huu wa 2018, amefananisha ICC na mshumaa, akisema mshumaa huo uliwashwa miaka 20 iliyopita kuangazia madhila dhidi ya binadamu na hivyo ni jambo jema kila mtu kuhakikisha unaendelea kuwaka.

Makao makuu ya Mahakama ya Kimataifa ya uhalifui -ICC- mjini THe Hague Uholanzi
Picha ya ICC-CPI
Makao makuu ya Mahakama ya Kimataifa ya uhalifui -ICC- mjini THe Hague Uholanzi

Kauli hii ya Rais huyu wa ICC inakuja wakati baadhi ya mataifa yakiwa yametangaza kujiondoa kwenye chombo hicho, ambapo miongoni mwao ni Ufilipino, Afrika Kusini na Burundi.

Ripoti hiyo pamoja na mambo mengine inataka ushirikiano zaidi kati ya ICC na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lina mamlaka ya kuwasilisha kisa au tukio lolote mbele ya mahakama hiyo ili liweze kufuatiliwa.

“ICC inaamini kuwa pale kuwepo kwa mawasiliano yenye mpango kati yake na Baraza la Usalama kwenye masuala ya maslahi kwa pande zote, iwe ya kimaudhui au ya hali ya tukio fulani, kutasaidia kuimarisha utekelezaji wa maazimio ya Baraza hilo kuhusu visa vya kufuatilia na hivyo kuchagiza vita dhidi ya ukwepaji sheria,” imesema ripoti hiyo.

Katika kikao hicho, wajumbe walipitisha azimio ambalo pamoja na mambo mengine linapongeza ripoti ya utendaji na kutaka nchi wanachama wa mkataba wa Roma wa mwaka 1998 ulioanzisha ICC wachangie mfuko unaotoa msaada kwa waathirika wa makosa ya uhalifu wa kivita.