Rais wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa Bi María Fernanda Espinosa amtembelea Papa Francis.

29 Oktoba 2018

Rais wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa Bi María Fernanda Espinosa, asubuhi hii amekutana na kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis mjini Vatican, nchini Italia , kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Bi Espinosa amenukuliwa akisema, “Asubuhi hii nimekutana na Baba Mtakatifu Papa Francis. Tumejadili masuala muhimu kuhusu uhamaji na wakimbizi. Pia tumezungumza kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, vijana na kazi na pia nafasi ya wanawake katika jamii. Tumejadili pia matatizo matatizo yanaletwa na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na plastiki. “

Kwa kutambua mchango wa Papa Francis katika imani na uongozi alioutoa katika masuala mbalimbali ya kidunia ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na kulinda mazingira, Bi Espinosa ameeleza Imani yake na ile ya nchi nyingi wanachama  wa Umoja wa Mataifa kuwa mshikamano wa kimataifa ndiyo njia pekee ya uhakika ya kueleza na kushughulikia matatizo na mahitaji ya kibinadamu.

Aidha Maria Fernanda Espinosa amesema, “ Ninapenda kuitumia fursa hii adhimu ya kukutana na Papa Francis kutambua umuhimu wa nafasi ambayo ameichangia tangu mwanzo alipoichukua nafasi hii ya upapa, katika kushughulikia masuala ya uhamaji na wakimbizi. Ndani ya Papa Francis tuna kiongozi wa kiroho ambaye anasimama kwa ajili ya utu na ambaye anahamasisha kuwa matatizo duniani yanapatiwa ufumbuzi.”

Vilevile taarifa inasema kuwa wakati wa mkutano wake na Papa Francis, Bi. Espinosa pia ameeleza juu ya nia yake ya kupatia kipaumbele haki za watu wa asili na masuala yanayowaathiri. Pia amesisitiza kuwa kipaumbele chake kingine wakati wa uongozi wake kitakuwa kukuza kazi zenye sitaha kwa msisitizo juu ya vijana na watu wenye ulemavu.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter