Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye Ngaïssona wa CAR akabidhiwa ICC

Makao makuu ya mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC huko The Hague, Uholanzi
UN /Rick Bajornas
Makao makuu ya mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC huko The Hague, Uholanzi

Hatimaye Ngaïssona wa CAR akabidhiwa ICC

Amani na Usalama

Hii leo, Patrice-Edouard Ngaïssona ambaye anatuhumiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita na dhidi ya binadamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, amekabidhiwa kwa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC huko The Hague, Uholanzi.

Kukamatwa kwa Ngaïssona na kukabidhiwa hii leo kutoka Ufaransa ambako alikamatwa tarehe 12 mwezi Disemba mwaka jana, kunafuatia kukamilika kwa taratibu zilizofuatia kutolewa tarehe 7 mwezi huo huo wa Disemba kwa hati ya kukamatwa na mahakama hiyo.

Msajili wa ICC, Peter Lewis ameshukuru mamlaka za Ufaransa na Uholanzi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha kukamatwa kwake na kukabidhiwa kwa mahakama hiyo yenye makao yake nchin Uholanzi.

ICC imesema itatangaza punde tarehe ya mashauriano ya awali ya kesi dhidi ya Ngaïssona  ambapo mahakama itathibitisha utambulisho wa mtuhumiwa na lugha ambayo itamwezesha kufuatilia mchakato mzima wa kesi dhidi yake na pia atajulishwa mashtaka yanayomkabili.

Makosa yanayomkabili Ngaïssona ni uhalifu wa kivita na uhalifu wa kibinadamu ambao anadaiwa kutenda katika maeneo tofauti nchini CAR kati ya tarehe 5 Disemba mwaka 2013 hadi Disemba 2014.

Mathalani mauaji, kutia watu korokoroni, utesaji, kukata watu viungo, kushambulia misafara ya magari na uporaji wa mali.

Mwaka jana wa 2018, Ngaïssona mwenye umri wa miaka 55, alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati tendaji ya shirikisho la soka barani Afrika, CAF.