Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walio kwenye msafara wa Amerika ya kati wanaweza kuwa hatarini:UNHCR

Wafanyakazi wa UNHCR wakisaidia watu katika mpaka wa Mexico na Guatemala ambao wamewasili na msafara wa wakimbizi na wahamiaji kutoka Honduras Oktoba 21, 2018
© UNHCR/Julio López
Wafanyakazi wa UNHCR wakisaidia watu katika mpaka wa Mexico na Guatemala ambao wamewasili na msafara wa wakimbizi na wahamiaji kutoka Honduras Oktoba 21, 2018

Walio kwenye msafara wa Amerika ya kati wanaweza kuwa hatarini:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limepeleka wafanyakazi wake huko kusini mwa Mexico kama njia mojawapo ya kukabiliana na janga la kibinadamu linaloweza kutokea wakati huu ambapo  maelfu ya watu wanaingia Mexico na Guatemala wakitokea Honduras.

 

Kauli hiyo imetolewa leo  na msemaji wa UNHCR Adrian Edwards wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi  ambapo amesema kuwa  kufikia jana watumishi 45 wa UNHCR wako katika mji wa Tapachula jimboni Chiapas nchini Mexico na wengine wako njiani kwenda kuungana nao.

Amesema “ timu zetu zinatoa misaada ya kiufundi na watendaji ili kuhakikisha wanaosaka hifadhi wanasajiliwa na kuweka  mfumo wa kuwatambua na kuwasaidia wale ambao wako katika hali ya kuhitaji msaada wa haraka na pia kuweza kutoa mahali pa kukaa.”

Msafara huo wa maandamano ambao unakadiriwa kuwa na watu 7,000 au zaidi ni wa pili kuandaliwa kutembea katika eneo hilo mwaka huu, ambapo wa kwanza  ulifanyika mwezi Aprili nchini Mexico.

Halikadhalika Bwana Edwards amesema nchini Guatemala, UNHCR inafuatilia hali ilivyo kwenye eneo la mpakani la Tecun Uman na zaidi ya yote“Wasiwasi wetu kwa sasa ni hali ya kibinadamu inayojitokeza pamoja na utekaji nyara na wasiwasi wa kiusalama katika maeneo ambako msafara huo utapitia. Kuweka utulivu ni jambo la dharura na ni muhimu kuwepo na sehemu maalum ya kuwapokea na pia mazingira sahihi kwa wasaka hifadhi na wale wanaotaka kuendelea na msafara.”

UNHCR inakumbusha mataifa kuwa baaadhi ya watu walioko katika msafara huo maisha yao yanaweza kuwa hatarini.