Marekani yatangaza kujitoa shirika la posta duniani, UPU

18 Oktoba 2018

Marekani imetangaza kujitoa katika shirika la posta duniani, UPU ndani ya mwaka mmoja ujao.

Taarifa za hatua hiyo ya Marekani zimethibitishwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UPU, Pascal Clivaz kupitia taarifa yake iliyotolewa hii leo huko Berne, Uswisi.

Bwana Clivas amesema notisi ya Marekani imewasilishwa jana Jumatano na Waziri wake wa Mambo ya Nje Mike Pompeo ambapo Marekani ambayo ni moja ya nchi anzilishi za UPU imesema kupitia notisi hiyo kuwa “barua hii ni ya kuarifu kuwa serikali ya Marekani inalaani katiba  ya UPU na hivyo basi inajiondoa kutoka shirika la posta duniani. Kujitoa huku kutakuwa rasmi mwaka mmoja tangu utakapopokea taarifa hii.”

Akizungumzia notisi hiyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa UPU amesema “hatua ya Marekani ni ya kusikitisha, Marekani ni miongoni mwa waanzilishi wa UPU na kwa miaka kadhaa imekuwa na mchango mkubwa katika ushirika huu. Hata hivoy tunaheshimu uamuzi wao ambao tunaamini umechukuliwa kwa uangalifu mkubwa.”

Hata hivyo Bwana Clivas amearifu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa UPU Bishar A. Hussein atasaka fursa ya kukutana na wawakilishi wa serikali ya Mareakni ili kujadili zaidi hatua hiyo.

Amesema UPU inasalia na azma  yake ya kutekeleza malengo yake ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa akisema, “hii ina maana kwamba tutashirikiana na wanachama 192, kuhakikisha kwamba kupitia mikataba ya UPU wanahudumia kila mtu ikiwemo Marekani.

Bwana Clivas amesema ana matumaini kuwa kupitia majadiliano ya dhati, wataweza kutatua masuala ambayo  yatafurahisha kila upande.

UPU ilianzishwa miaka 144 iliyopita na ina jukumu la kusafirisha vifurushi kwa wanachama kwa mujibu wa kanuni ilizowekwa na wanachama.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter