Acheni kuchunguza iwapo msichana ana bikira au la- UN

Wasichana hawapaswi kufanyiwa kitendo hicho dhalili na kisicho na misingi yoyote ya kitabibu au kisayansi
UN /Albert González Farran
Wasichana hawapaswi kufanyiwa kitendo hicho dhalili na kisicho na misingi yoyote ya kitabibu au kisayansi

Acheni kuchunguza iwapo msichana ana bikira au la- UN

Afya

Mashirika ya Umoja wa Mataifa leo yametoa taarifa ya pamoja yakitaka kutokomezwa kitendo cha kupima iwapo mtoto wa kike au msichana ana bikira, yakisema kitendo hicho ni dhalili na kinyume cha haki za binadamu.

Uchunguzi huo wa iwapo mtoto wa kike au msichana ana bikira, yaelezwa ina lengo la kubaini iwapo amewahi kujamiiana au la ambapo mashirika hayo ikiwemo lile la afya duniani, WHO, lile la kushughulikia masuala ya wanawake, UN-Women na ofisi ya haki za binadamu wamesema hakuna msingi wowote wa kisayansi au kitabibu.

“Hakuna uchunguzi wowote ambao unaweza kuthibitisha iwapo msichana au mwanamke amejamiiana na kuwepo kwa bikira kwa mwanamke au msichana hakuwepo kudhihirisha iwapo wamejamiiana au ameanza kufanya kitendo hicho,” imesema taarifa hiyo ya pamoja iliyotlewaleo huko Geneva, Uswisi.

Bila kutaja mataifa ambako bado kitendo hicho kinafanyika, taarifa hiyo inasema kuwa uchunguzi wa bikira hudaiwa kufaniyka ili kukagua hali ya manusura wa kitendo cha ubakaji, ikisema hata hivyo kutokana na taratibu zenyewe za uchunguzi kutokuwa na msingi wa kisayansi, matokeo yanaweza kuwa athari hasi kwenye taratibu za kesi ya ubakaji kwa kumpendelea mbakaji.

Uchunguzi wa iwapo msichana au mwanamke ana bikira au la unaweza kuathiri ustawi wa kimwili, kisaikolojia na kijamii kwa kundi hilo na zaidi ya yote kitendo hicho kinaendeleza fikra potofu kuhusu hali ya kimwili ya mwanamke na suala la ukosefu wa usawa wa kijinsia.

Waathirika wengine wa kitendo hiki ni wanawake wafungwa ambao hukaguliwa kuona iwapo wanajihusisha na ngono au la wanapokuwa gerezani huku kwingineko uchunguzi ukifanyika kwa madai ya kuona iwapo mhusika anaweza kuajiriwa au kuolewa.

Yakifafanua kuhusu ukiukaji wa haki ya binadamu kupitia kitendo hicho dhalili, mashirika hayo yamesema “uchunguzi wa iwapo msichana au mwanamke ana bikira au la unaweza kuathiri ustawi wa kimwili, kisaikolojia na kijamii kwa kundi hilo na zaidi ya yote kitendo hicho kinaendeleza fikra potofu kuhusu hali ya kimwili ya mwanamke na suala la ukosefu wa usawa wa kijinsia,” imesema taarifa  hiyo.

Imeenda mbali na kuongeza kuwa uchunguzi huo unaweza kuwa na maumivu makali, unadhalilisha na unatisha kwa kuzingatia kuwa taratibu za kufanyika kwake zinaweza kuwa hatarishi, kinyume na maadili kwa madaktari au watoa huduma ya afya kuzitekeleza. Taratibu hizo katu hazipaswi kufuatwa.

Akinukuliwa kwenye taarifa hiyo, Dkt. Nothema Simelela ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa WHO akihusiska na masuala ya familia, watoto na barubaru amesema “wataalamu wa afya ndio wanaweza kuwa mawakala wa mabadiliko.”

Dkt. Simelela amesema kwa msaada wa mifumo ya afya na serikali, wahudumu hao wanaweza kutambua kuwa uchunguzi wa bikira hauna msingi wowote wa kisayansi au kitabibu.  Hivyo wanaweza kukataa kutekeleza kitendo hicho na kuelimisha umma kuhusu suala hilo.

Amesema kwa kufanya hivyo, “watakuwa wanazingatia kiapo chao cha kimaadili cha kutomuumiza mtu yeyote na kulinda haki za wasichana na wanawake wanaokuwa wanawahudumia.”