Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki na afya ya wakimbizi, wahamiaji na wasio na utaifa inatakiwa kulindwa wakati wa kushughulikia COVID-19

Wakimbizi wa ndani walio katika jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC
© UNFPA DRC
Wakimbizi wa ndani walio katika jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC

Haki na afya ya wakimbizi, wahamiaji na wasio na utaifa inatakiwa kulindwa wakati wa kushughulikia COVID-19

Wahamiaji na Wakimbizi

Taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari iliyotolewa hii leo na Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la wahamiaji, IOM, la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la afya WHO imetoa wito kwa dunia kulinda haki na afya ya wakimbizi, wahamiaji na wasio na utaifa katika wakati huu wa mapambano dhidi ya virusi vya corona, COVID-19.

“Katika wakati huu wa janga la COVID-19, sisi wote tuko hatarini. Virusi vimeonesha kuwa havibagui, lakini wakimbizi wengi, wale waliofurushwa, wasio na utaifa na wahamiaji wako katika hatari kubwa.” Imesema taarifa hiyo. 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa robo tatu ya wakimbizi wote duniani na wahamiaji wengi wako katika ukanda wa nchi zinazoendelea ambako mifumo ya afya tayari imezidiwa na haina uwezo. Wengi wanaishi katika kambi, makazi na vituo ambako tayari kuna msongamano mkubwa, ambako wanakosa huduma ya afya, maji safi na salama na huduma ya kujisafi.

Hali ya wakimbizi na wahamiaji waliohifadhiwa katika maeneo rasmi na yasiyo rasmi, katika maeneo finyu na yasiyo safi, ni ya kutia wasiwasi. 

“Kwa kuzingatia athari mbaya ambazo zinaweza kusababishwa na mlipuko wa COVID-19, wanatakiwa kuachiwa bila kuchelewa.  Watoto wanaohama na familia zao na wale waliowekwa kizuizini bila msingi wa kisheria wa kutosha wanapaswa kuachiliwa mara moja.” Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yamesisitiza.

Aidha mashirika hayo ya Umoja wa Mataufa yamesema, COVID-19 inaweza kudhibitiwa ikiwa tu kuna njia inayojumuisha ambayo inalinda haki za kila mtu za maisha na afya.

Wahamiaji na wakimbizi wako katika hatari ya kutengwa, unyanyapaa na ubaguzi, haswa wanapokuwa hawana nyaraka. Kuepuka janga, serikali lazima zifanye yote yanayoweza kulinda haki na afya ya kila mtu. Kulinda haki na afya ya watu wote kwa kweli kutasaidia kudhibiti kuenea kwa virusi.

Ni muhimu kwamba kila mtu, pamoja na wahamiaji wote na wakimbizi, wahakikishiwe upatikanaji sawa wa huduma za afya na wajumuishwe katika kushughulikia COVID-19, pamoja na kuzuia, kupima na matibabu. Kujumuishwa hakutasaidia kulinda haki za wakimbizi na wahamiaji tu, bali pia kutasaidia kulinda afya ya umma na kudhibiti kuenea kwa COVID-19 ulimwenguni. Wakati mataifa mengi yanalinda na kuwakaribisha wakimbizi na idadi ya wahamiaji, mara nyingi hawakuwa na vifaa vya kushughulikia majanga kama kama COVID-19. Kuhakikisha wakimbizi na wahamiaji wanapata huduma za afya za kitaifa, nchi zinaweza kuhitaji msaada wa kifedha zaidi. Hapa ndipo taasisi za kifedha za ulimwengu zinaweza kuchukua jukumu kubwa katika kufanikisha upatikanaji wa fedha. 

Wakati nchi zinafunga mipaka yake na kubana shughuli za kuvuka mipaka, kuna njia za kushughulikia ubanaji mipaka katika namna ambayo inaheshimu haki za kimataifa za binadamu na viwango vya ulinzi wa wakimbizi ikiwemo kuwaeka watu kwenye karantini na pia kuwapima afya zao.