Jumuiya ya kimataifa watazameni wanawake wa vijijini- UN-Women

15 Oktoba 2018

Hii leo Oktoba 15 katika kuadhimisha sikuya kimataifa ya wanawake wa vijijini duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya wanawake, UN Women, limeitaka jumuiya ya kimataifa kufanya kazi na wanawake wa vijijini na wasichana kila mahali na kuwekeza katika miundombinu endelevu, huduma na ulinzi, vitu ambavyo vinaweza kubadilisha maisha yao, ustawi na ujasiri wao.

UN-Women inasema katika nchi nyingi duniani kote, wanawake wa vijijini na wasichana wanakabiliwa na changamoto za miundombinu, huduma na kulindwa ikisema uwepo wa changamoto hizi unahitaji mabadiliko makubwa ili zisiweze kuendelea kuwepo na kukandamiza maisha ya wanawake na wasichana.

“Wanawake wa vijijini ni asilimia 43 ya nguvu kazi ya kilimo katika nchi zinazoendelea na utumikishaji watoto upo kwa wingi katika maeneo ya vijijini ambako wasichana ni sehemu muhimu ya nguvu kazi katika kilimo,” imesema taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini New York, Marekani.

UN-Women imeongeza kuwa asilimia 80 ya familia zote kwenye nchi hizo, wanawake na wasichana wanawajibika kuteka maji huku wakiwa hawana maji salama ya kunywa. “kazi hii ni ngumu na inakuwa ngumu zaidi wakati upungufu wa maji unapoongezeka. Safari ya kufuata maji pia inakuja na hatari nyingi. Bila maji safi na salama, wanawake wa wasichana wanakuwa hatarini kupata magonjwa pamoja na hatari nyingine. Mambo haya pia huathiri uwezo wao wa kupata elimu bora, kupata kipato na kuweza kuzunguka huku na kule kwa uhuru,” imesema taarifa hiyo.

Kama hiyo haitoshi, wanawake na wasichana hutumia muda mrefu kusaka nishati wakati mwingine hadi usiku wa mananeno na katika ambazo wanategemea sana nishati kama mkaa, kuni, kinyesi cha mifugo au mabaki ya mimea kwa ajili ya kupikia, wanawake 6 kati ya 10 wanapoteza maisha katika vifo vya mapema kupitia uchafuzi wa hali ya hewa majumbani.

Kwa mantiki hiyo UN-Women inasema miundombinu endelevu, huduma na kulindwa na jamii ni mambo muhimu ili kuweza kuendelea sambamba na kuboresha hali kunaweza kuleta unafuu wa haraka na faida za muda mrefu.

Mathalani, kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kunaleta ongezeko katika elimu ya wasichana wakati watoto wanapokaa muda zaidi shuleni, pia kuongeza wanawake wanaolipwa kuzalisha bidhaa na kutoa huduma. Kwa msingi huo kufikisha mabomba ya maji katika jamii za vijijini ni kipaumbele muhimu chenye faida nyingi.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter