Baada ya kupata stadi, mkimbizi Yunus anahitaji pembejeo na ardhi ili akwamue maisha yake

17 Oktoba 2018

Mradi wa pamoja wa mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa na serikali  ya Uturuki umeanza kuwajengea uwezo wa kijamii na kipato wakimbizi wa Syria waliosaka hifadhi nchini humo kutokana na vita vilivyodumu nchini mwao kwa miaka saba sasa. 

Katika jimbo la Gaziantep, nchini Uturuki, Yunus Yunus mkimbizi kutoka Syria akikagua shamba lake la mizabibu. Fikra zake ni Aleppo, mji aliokimbia ambako kila siku makombora yapatayo manane yaliangushwa na kusababisha vifo na majeraha.

Yunus anasema alilazimika kukimbilia Syria kwa sababu lukuki, mosi alijeruhiwa na mbavu zake zilizunjika na pili alihofia usalama wa familia yake hususan watoto wake wawili wa kiume alihofia kuwa watatekwa tena na alazimike kulipa fedha kuwakomboa.

Sasa hapa Uturuki angalau Yunus na wakimbizi wengine 900 wana uhakika kwa kuwa mradi unaotekelezwa na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO na lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwa kushirikiana na serikali ya Uturuki, umewapatia ujuzi wa  kilimo.

Mafunzo ya FAO yameleta msaada mkubwa kwa kuwa “nadharia tunayofundishwa inajumuisha masomo ya jinsi ya kuhifadhi na kupanda mazao na pia kutunza mashamba yetu. Katika utekelezaji tunapelekwa mashambani. Tunapanda mazao na kujifunza jinsi ya kutunza mizabibu na pitsacho. Nimenufaika na hili.”

Sasa Yunus yuko kwenye shamba lake la mizeituni akisema, “iwapo mtu atanifadhili au anipatie eneo la ardhi pamoja na pembejeo za kilimo kama vile mbegu na mbolea, ninaweza kujitegemea. Nitanufaika zaidi na mradi huu na ninaweza kusaidia wengine.”

Uturuki ambayo sasa inakosa nguvukazi katika sekta ya kilimo na mifugo inatarajia kuwa mradi  huu wa mafunzo utawezesha wakimbizi kupata stadi na hivyo kuchangia katika utendaji wa kazi na pia kujenga mnepo kwa jamii zinazowahifadhi.

Idadi kubwa ya wakimbizi wa Syria waliohama nchi yao wanaishi Uturuki.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud