Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka ukurugenzi serikalini Syria hadi kilimo cha kibarua Uturuki

Watoto wakitafuta maji katika katika mji ulioharibiwa kwa vita, Aleppo
UN
Watoto wakitafuta maji katika katika mji ulioharibiwa kwa vita, Aleppo

Kutoka ukurugenzi serikalini Syria hadi kilimo cha kibarua Uturuki

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na serikali ya Uturuki wameungana kuwafundisha stadi za kilimo zaidi ya wasyria 900 pamoja na baadhi ya wenyeji waliowapokea wakimbizi katika nchi hiyo ambayo imepokea zaidi ya wakimbizi milioni 3.5 kutoka Syria. 

Yunus anaonekana anapalilia magugu katika shamba moja nchini Uturuki. Anasema hataki kukumbuka alilyoyapitia kiasi kwamba anaogopa hata kuangalia mpaka unaozitenganisha Syria na Uturuki.

Hata hivyo sasa akiwa ugenini, Yunus ni mmoja wa mamia ya wakimbizi kutoka Syria ambao wanafaidika na mafunzo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa shirika la chakula na kilimo duniani FAO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na serikali ya Uturuki.

Ni mafunzo yanayowapatia stadi za maarifa ya yanayohitajika katika sekta ya kilimo nchini Uturuki ambako wanapata hifadhi.

“Ingawa hapa maisha ni magumu, lakini ni bora kuliko kuishi katika mabomu bila usalama”

Yunus alikuwa anaishi mashariki mwa mji wa Aleppo katika wilaya ya El Helou nchini Syria, , taifa ambalo limesambaratishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2011. Anasema kwa siku yalilipuka mabomu hadi manane. Alitoroka Aleppo akiwa amejeruhiwa na kuvunjika mifupa ya mbavu.

“Nilikuwa mfanyakazi wa serikali, cheo cha ukurugenzi. Sikuwa nafahamu lolote kuhusu kilimo. Tulishiriki mafunzo ya FAO, kwanza kinadharia na  baadaye tunapelekwa shambani kujifunza kuhusu kupanda na kutunza shamba”

Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, wakimbizi wanafanya kazi katika mashamba ya wenyeji na kujipatia ujira wa kutunza familia zao. Yunus ana familia ya watoto sita na wawili kati yao ni wenye ulemavu.

Mradi ukiwa unaingia katika hatua yake ya pili, mamia zaidi ya wakimbizi kama Yunus wanaweza kujenga mstakabali ulio imara na salama wa maisha yao ya baadaye.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.