Uhamiaji wa ndani umesahaulika licha ya manufaa yake- SOFA

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya chakula na kilimo duniani, SOFA imeonyesha jinsi ambavyo uhamiaji mashambani ulivyo na manufaa lakini mara nyingi husahaulika.
Ripoti hiyo ikiwa imeandaliwa na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO inasema bayana kuwa uhamiaji ni jambo ambalo mtu anachagua, inaweka gharama na faida zake pamoja na athari zake zitokanazo na uamuzi wa uwekezaji muhimu katika kuendeleza maeneo ya vijijini.
Ikiwa imejikita zaidi na uhamiaji wa ndani, ripoti inasema kuwa ingawa uhamiaji wa kimataifa umekuwa ukigonga vichwa vya habari, uhamiaji wa ndani ya nchi umekuwepo zaman a zama ambapo zaidi ya watu bilioni 1 kote duniani wamekuwa wahamiaji ndani ya nchi zao.
Ni kwa mantiki hiyo ripoti inataka sera thabiti ambazo siyo zinalenga kupunguza au kuchochea mwelekeo wa uhamiaji bali kuongeza manufaa ya kiuchumi na kijamii na vile vile kupunguza gharama kwa wahamiaji na jamii zao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Jose Graziano da Silva ametilia mkazo huo akisema ‘Uhamiaji usichukuliwe kama suala la dharura. Imekuwa sehemu ya será za maendeleo kwa muda mrefu. Mataifa mengi duniani kwa sasa yamefaidika sana kutokana na uhamiaji. Watu wengi wanaohama , ni vijana tena walioelimika na wamekuwa wakisaidia mataifa mengi kuendelea.Kwa hivyo tusichukulie kama uvurugaji katika ngazi ya kimataifa na kushughulikia wahamiaji kama suala la dharura.Uhamiaji waweza kuwa jambo zuri ikiwa umechukuliwa katika njia inayofaa kwa kukaribisha wahamiaji katika makazi yao mapya. Kwa njia nzuri.”
Ripoti vilevile inasema kuwa uhamiaji unafaa kuwa chaguo la mtu na wala sio ulazima, ikiongeza kuwa sera za kuendeleza uhamiaji, kilimo pamoja na sehemu za mashambani zinafaa ziwe zinasaidia uhamiaji ulio na utaratibu, wa amani na wa wakati.
SOFA inasema katika mataifa yenye kipato cha chini watu ambao wamehama kutoka maeneo ya ndani mwa nchi zao wakitafuta maisha mazuri, wana nafasi mara tano zaidi ya kuweza kuhamia nje ya nchi kuliko wale ambao hawajahama kwa njia yoyote ile.