Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo kikisimamiwa na wanawake kinakuwa na tija zaidi- FAO

Wanawake wakiuza nyanya katika soko nchini Ghana barani Afrika.
FAO/Cristina Aldehuela
Wanawake wakiuza nyanya katika soko nchini Ghana barani Afrika.

Kilimo kikisimamiwa na wanawake kinakuwa na tija zaidi- FAO

Wanawake

Ukosefu wa usawa wa kijinsia katika sekta ya kilimo barani Afrika, unakwamisha maendeleo ya kutokomeza njaa barani humo, amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa Jose Graziano da Silva. 

Akizungumza kando mwa mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New York, Marekani, Bwana da Silva amesema pengo hilo la usawa wa kijinsia ni lazima lishughulikiwe haraka ili kuondoa vikwazo hivyo vya kutokomeza njaa.

Amesema “tunahitaji kutambua vyema na kutumia ipasavyo mchango wa wanawake katika uhakika wa upatikanaji wa chakula na lishe. Hivyo ni lazima tuondoe pengo la usawa wa kijinsia barani Afrika.”

Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO ametoa kauli hiyo baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya pamoja ya shirika hilo na Muungano wa Afrika, AU ikiangazia mtazamo wa kijinsia katika mifumo ya uzalishaji wa mazao ya chakula.

Ripoti hiyo inafuatia tathmini ya kina ya mipango ya 38 ya  kitaifa ya kilimo barani kwa lengo la kutambua ni kwa jinsi gani usawa wa kijinsia au pengo la usawa huo vinakwamisha au kusongesha uzalishaji wa chakula barani Afrika, ambapo nchi 40 zilihusika.

Ilibainika kuna pengo kubwa la takwimu juu ya ushiriki wa wanawake katika sekta ya kilimo ambapo Bwana da Silva ametaka kuwepo kwa uwakilishi bora zaidi wa wanawake katika michakato ya uongozi na utoaji maamuzi pamoja na fursa za kumiliki ardhi, rasilimali fedha, huduma na mipango ya ulinzi wa kijamii kwa wanawake wa vijijini.

Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva.
FAO/Giuseppe Carotenuto
Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva.

 

 

Shirika hilo linasema iwapo pengo hilo la jinsia litaondolewa, uzalishaji na ulaji wa chakula unaweza kuongezeka kwa hadi asilimia 10 na hivyo kupunguza umaskini kwa hadi asilimia 13.

“Ripoti inataka mapinduzi makubwa ya takwimu za kijinsia katika sekta ya kilimo ili zichangie katika sera bora na kuinua kiwango cha mipango, ufuatiliaji na uwajibikaji katika sekta hioyo,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO.

Amesema ushahidi unaonyesha kuwa pindi wanawake wanawezeshwa, mashamba yanakuwa na mazao bora zaidi, maliasili zinasimamiwa vizuri, lishe inakuwa bora na maisha ya jamii yanakuwa ya uhakika.

FAO inasema katika baadhi ya nchi za Afrika, wanawake ni takribani asilimia 60 ya nguvukazi inayotumika kwenye kilimo cha kaya, wakiwajibika na upanzi wa mboga, uhifadhi wa mavuno na ufugaji wa Wanyama kama vile mbuzi na kondoo. Wanawake pia wanawajibika kwa lishe ya familia kupitia jukumu lao la kuandaa mlo wa familia.