Twashukuru wanahabari wameachiwa huru lakini hali bado si shwari Mynmar

7 Mei 2019

Umoja wa Mataifa umeeleza msimamo wake kufuatia kuachiliwa huru kwa waandishi wa habari wawili waliokuwa wamefungwa nchini Myanmar.

Waandishi hao wa shirika la habari la Reuters, ni Kyaw Soe Oo na Wa Lone ambao wamepatiwa msamaha na Rais wa Myanmar, Win Myint walihukumiwa kifungo cha miaka 7 gerezani mwaka jana kwa makossa ya kuvunja sheria ya kutoboa siri za nchi walipokuwa wakiripoti taarifa za mauaji ya warohingya yaliyotekelezwa na majeshi ya Mynmar mwezi septemba mwaka 2017.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amenukuliwa kupitia msemaji wake akikaribisha kuachiliwa huru kwa wanahabari hao ambao ni washindi wa tuzo ya mwaka huu ya uhuru wa vyombo vya habari ya UNESCO na Guillermo Carmo.

Warohingya ambao ni kabila kutoka jimbo la Rakhine nchini Myanmar, hawana uraia na hawana utambulisho wowote. Hapa ni Cox's Bazar nchini Bangladesh wakiwa hawajui hatma ya kurejea nchini mwao.
K M Asad/UN
Warohingya ambao ni kabila kutoka jimbo la Rakhine nchini Myanmar, hawana uraia na hawana utambulisho wowote. Hapa ni Cox's Bazar nchini Bangladesh wakiwa hawajui hatma ya kurejea nchini mwao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay naye amekaribisha hatua hiyo akisema ni bora kwa wao wenyewe na wapendwa wao na pia ni hatua chanya kuelekea uhuru wa vyombo vya habari nchini Myanmar.

“UNESCO inakumbusha kuwa kitendo cha wanahabari kufanya kazi yao bila hofu ya visasi ni hatua muhimu katika demokrasia zinazofanya kazi yake ipasavyo,” amesema Bi. Azoulay akiongeza kuwa kupitia ujasiri na kujitoa kwao, Kyaw Soe Oo na Wa Lone ni hamasa kwa wale wote ambao wanahaha kutetea uhuru wa vyombo vya habari.

Hata hivyo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR kupitia msemaji wake Ravina Shamdasani imerejela ripoti yake ya mwezi Septemba mwaka jana iliyotolewa punde tu baada ya hukumu ya wanahabari hao.

“Ni habari njema kuwa wameachiwa huru lakini kwanza kabisa hawakupaswa kukamatwa na kuhukumiwa. Bado tuna hofu kubwa juu ya kuwepo kwa mianya kwenye mchakato wa mahakama ambao ulisababisha wafungwe, na kesi yao ni mfano wa kesi nyingi ambazo mkwamo wa kisheria umekuwa sababu za kubinya uhuru wa vyombo vya habari,” amesema Bi. Shamdasani.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter