Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL bado ni tishio, juhudi za pamoja zahitajika kulisambaratisha- Voronkov

Uharibifu mkubwa uliofanyika Iraq mji wa Mosul ambako watu walipoteza maisha mikononi mwa kundi hilo.
UNICEF/Sparks
Uharibifu mkubwa uliofanyika Iraq mji wa Mosul ambako watu walipoteza maisha mikononi mwa kundi hilo.

ISIL bado ni tishio, juhudi za pamoja zahitajika kulisambaratisha- Voronkov

Amani na Usalama

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ugaidi, Vladmir Voronkov amesema hayo amesema mtandao wa magaidi wa ISIL unaendelea kuendesha operesheni zake kisiri huko mashinani nchini Syria na Iraq na kutishia harakati za kuleta utulivu nchini humo.

Vladmir Voronkov, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia ofisi ya kupambana na ugaidi akihutubia Baraza la Usalama
UN Photo/Manuel Elías
Vladmir Voronkov, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia ofisi ya kupambana na ugaidi akihutubia Baraza la Usalama

Akiwasilisha ripoti ya 8 ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mbele ya Baraza la Usalama la umoja huo hii leo jijini New York, Marekani kuhusu tishio la ISIL  kwenye amani na usalama duniani, Bwana Voronkov amesema magaidihao wanaendelea kujiimarisha  hususan Iraq na Syria ambako yaripotiwa wanamiliki wapiganaji kati ya 14,000 hadi 18,000 wakiwemo 3,000 ambao ni wapiganaji wa kigeni.

“Licha ya kuwa na operesheni za kisiri, utawala wa ISIL umeendelea kuwa na ushawishi na kuendeleza nia yake ya kufanya mashambulio kimataifa na hivyo kuendeleza malengo yao ya ugaidi,” amesema Voronkov.

Kuhusu uwezo wa kifedha wa ISIL, Bwana Voronkov amesema licha ya kupoteza mapato yao kutokana na kudhibitiwa kwenye baadhi ya maeneo, bado kundi hilo linaweza kusongesha operesheni zake kwa kutumia akiba ya fedha ambayo ni kati ya dola milioni 50 hadi milioni 300.

Myazidi kutoka Sinjar  nchini Iraq ambaye alitekwa nyara na kikundi cha ISIL, hapa yuko kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani  ya Mamilyan  huko Akre, nchini Iraq
Giles Clarke/ Getty Images Reportage
Myazidi kutoka Sinjar nchini Iraq ambaye alitekwa nyara na kikundi cha ISIL, hapa yuko kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Mamilyan huko Akre, nchini Iraq

“Vikundi vya ISIL vyaripotiwa kupata mapato kutokana na shughuli za kihalifu,” amesema Bwana Voronkov akienda mbali zaidi kutaja jinsi ambavyo kundi hilo linatandaza operesheni zake maeneo mbalimbali duniani.

Mathalani eneo la Kusini-mashariki mwa Asia, ripoti imebaini ongezeko la vijana na wanawake wanaojiunga na operesheni za ISIL lijulikanalo pia kama Da’esh kwenye ukanda huo akisema ni changamoto ambazo wanatumia mfumo wa kukabili changamoto hizo.

Ametoa wito kwa nchi wanachama kusaidia harakati za kukabiliana na ugaidi akitaja zaidi suala la wapiganaji wa kigeni.

Ni kwa mantiki hiyo amesema katika ripoti hiyo ya leo, Katibu Mkuu wa UN ameisihi ofisi hiyo iwe na jukwaa ambamo kwalo litaweza kutoa fursa kwa watu kupata ujuzi na taarifa husika kuhusu mbinu bora za kukabiliana na ugaidi na hivyo kuimarisha uwezo wa nchi wanachama kukabiliana na ugaidi.

“Hii ni muhimu sana kwenye kushughulkia mmiminiko wa wapiganaji wa kigeni, wapiganaji wanaohamia maeneo mengine na wale wanaorejea nyumbani kutoka kwenye uwanja wa mapigano.

Amekumbusha kuwa tishio la ugaidi bado ni changamoto kubwa duniani na hivyo juhudi za pamoja za kimataifa zinatakiwa ili kuweza kukabiliana nalo.