Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda inaendelea kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa-Dkt Rugunda

Waziri Mkuu wa Uganda, Ruhakana Rugunda akihutubia Mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, tarehe 28 Septemba 2019
UN Photo/Cia Pak
Waziri Mkuu wa Uganda, Ruhakana Rugunda akihutubia Mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, tarehe 28 Septemba 2019

Uganda inaendelea kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa-Dkt Rugunda

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Waziri Mkuu wa Uganda Dkt Ruhakana Rugunda akihutubia mjadala mkuu wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mkutano wa 74, UNGA74, miongoni mwa mengi, amesema Uganda inaendelea kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa kwani ndiyo njia ya kufikia malengo dunia iliyojiwekea.

Dkt Ruhakana akitoa mfano wa ushirikiano wa hivi karibuni ameeleza kuhusu mapambano ya dhidi ya Ebola akisema, “mlipuko wa hivi karibuni ni  ukumbusho wa maeneo ambayo nchi katika ukanda zikishirikiana na jumuiya ya kimataifa, zinaweza kufanya kazi pamoja kugundua, kutathimini, kutaarifu na kushughulikia tishio hilo la kiafya. Uganda imeshiriki katika juhudi za namna hiyo na tunashukuru kwa msaada wa kimataifa katika kushughulikia mlipuko wa hivi karibuni katika ukanda wetu. Ninapenda kuipongeza Uganda kwa utayari na wake katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika eneo hili.”

Akizungumzia suala la kupokea wakimbizi, Dkt Rugunda amesema Uganda imeendelea na será yake ya mlango wazi kwa wakimbizi na hivi sasa nchi yake ni mwenyeji wa zaidi ya wakimbizi milioni 1.3, idadi kubwa zaidi katika bara la Afrika.

“Njia yetu ya kupokea wakimbizi imejikita katika roho yetu ya uafrika, ambapo tunawaona wakimbizi kama ndugu na dada zetu wanaokimbia migogoro na mafadhaiko, na ambao kwanza wanatafuta amani na usalama.” Amesisitiza Dkt Rugunda.

Hata hivyo Waziri Mkuu huyo wa Uganda ameeleza kuwa uwepo wa wakimbizi nchini mwake umekuwa na athari kwa mazingira akieleza kuwa kuanzia misitu imekatwa ili kupata miti ya kujenga nyumba za wakimbizi, kuni, na hata dawa.

Dkt Rugunda ameeleza kuwa, “inakadiriwa kuwa hekta 15,000 za misitu na uwanda wa savanna vimepotea kutokana na uwepo wa makazi ya wakimbizi.”

Kutokana na hali hiyo Dkt Rugunda ameitaka jumuiya ya kimataifa kuendeleza ushirikiano katika suala la wakimbizi ili kuzisaidia nchi zinazowapokea.

Kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi Dkt Rugunda amesema Uganda haijasazwa katika nchi zinazoathirika na mabadiliko ya tabianchi kwani imeshuhudia ukame wa muda mrefu, kuyeyuka kwa barafu katika mlima wake mrefu wa Ruwenzori, mafuriko, mvua zisizotabirika na maboromoko ya ardhi.

Aidha katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu Dkt Rugunda ameeleza namna Uganda inavyohakikisha inakamilisha mpango wake wa kila mwananchi kuwa na bima ya afya bila kujali hali yake ya maisha.