Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili dhidi ya wanawake Uganda sio majumbani tu hata vyuoni

Melisa Kyeyune wa Uganda, mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika masuala ya maendeleo kwenye chuo kikuu cha Martyrs, amehudhuria mkutano kuhusu utokomezaji wa ukatili dhidi ya wanawake,UNGA73
UN News/Flora Nducha
Melisa Kyeyune wa Uganda, mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika masuala ya maendeleo kwenye chuo kikuu cha Martyrs, amehudhuria mkutano kuhusu utokomezaji wa ukatili dhidi ya wanawake,UNGA73

Ukatili dhidi ya wanawake Uganda sio majumbani tu hata vyuoni

Wanawake

Tatizo la ukatili wa kijinsia ni kubwa duniani kote ndio maana Umoja wa Mataifa umelivalia njuga ili kuhakikisha ukatili huo unakomeshwa, lakini pia lengo namba 5 la maendeleo endelevu yaani SDG’s lihusulo usawa wa kijinsia linatimia ifikapo  2030.

Hata hivyo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kiwango cha ukumbwa wa tatizo kinatofautiana kutoka taifa moja hadi jingine. Nchini Uganda takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha asilimia 50 ya wanawake na wasichana walio katika mahusiano wanakabiliwa na aina fulani ya ukatili wa kijinsia.

Melisa Kyeyune raia wa Uganda ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika masuala ya maendeleo kwenye chuo kikuu cha Martyrs, amekua akihudhuria mkutano kuhusu utokomezaji wa ukatili dhidi ya wanawake uliofanyika kandoni mwa mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, na anasema

(SAUTI YA MELISA KYEYUNE)

“Ukatili wa kijinsia nchini Uganda kwa bahati mbaya unafanyika katika  sekta zote ikiwemo katika vyuo vikuu. Na hata kumekuwepo matukio ya wanawake kuuawa na wapenzi wao kwenye mazingira ya chuo kikuu.”

Na ili kukomesha hali hiyo Melisa anatoa wito

(SAUTI YA MELISA KYEYUNE)

“Kwanza wanaume ni lazima wawaheshimu wanawake zaidi, lazima wawaheshimu kama binadamu wenzao , na pili wanawake waelimishwe kuhusu haki zao na kila mtu ni lazima aelimishwe kwamba lengo la maendeleo endelevu namba 5 linachagiza usawa wa kijinsia.”