Baada ya jando ndio nilipatiwa viatu- Dkt. Kikwete

21 Septemba 2018

Kwa mara ya kwanza nilivaa viatu baada ya kutoka jandoni, ni kauli ya Rais Mstaafu wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete aliyotoa wakati akizungumzia kilichomo kwenye kitabu chake Safari yangu kutoka mwanafunzi aliyekwenda shule peku hadi Urais, kitabu kitakachozinduliwa hivi karibuni.

Katika moja ya kumbi za Chuo Kikuu cha New York, mjini New York jijini Marekani, Dkt. Jakaya Kikwete akisimulia hadhara iliyohudhuria tukio lake la kusoma kwa mara ya kwanza kitabu cha simulizi ya maisha yake, kuanzia utotoni hadi Urais.

Dkt. Kikwete alisimulia kwa lugha ya kiingereza akieleza majukumu yake kisiasa, jeshini na pia serikali na ndipo aliulizwa na Anold Kayanda wa Idhaa ya Kiswahili sababu ya kupatia kitabu chake jina la safari yangu-kutoka mwanafunzi mtembea peku hadi Urais. 

Dkt. Kikwete akasema, “Nilipata viatu nilipotoka jandoni...Raba. Nikipokwenda shule Mwalimu akaniambia kesho usije navyo kila mtu hana viatu hapa” 

Na vipi aliweza kukabili changamoto hizo hadi kuwa Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi 2015? Dkt. Kikwete akafunguka akisema kuwa, “Kitu muhimu wazazi wawasaidie watoto wao kusoma an watoto waweke bidii katika kusoma”

Dkt. Kikwete ambaye sasa ni mjumbe wa majopo ya ngazi ya juu ya Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la kuchangia elimu na pia masuala ya lishe, amesema kitabu chake ingawa kimeandaliwa kwa lugha ya kiingereza, tayari mchakato kukitafsiri kwa Kiswahili unaendelea. 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud