Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maambukizi ya kifua kikuu yalipungua 2017: WHO

Wanawake wawili ambao wanapata matibabu ya kifua kikuu mjini Addis Ababa , Ethiopia.
The Global Fund/John Rae
Wanawake wawili ambao wanapata matibabu ya kifua kikuu mjini Addis Ababa , Ethiopia.

Maambukizi ya kifua kikuu yalipungua 2017: WHO

Afya

Ripoti mpya ya  shirika la afya ulimwenguni WHO kuhusu hali ya ugonjwa wa  kifua kikuu duniani, TB  inasema kuwa  idadi ya watu waliougua kifua kikuu au kufariki dunia mwaka jana  ilikuwa ni ndogo ingawa bado mataifa mengi hayachukui  hatua za kutosha kuweza kutokomeza ugonjwa huo  ifikapo mwaka wa 2030.

Ikiwa imetolewa leo mjini New York, Marekani, ripoti inasema kuwa licha ya  juhudi duniani ambazo ziliweza kuzuia vifo vya watu milioni 54 kutokana na kifua kikuu tangu mwaka wa 2000, bado  TB inasalia kuwa ugonjwa hatari wa kuambukiza.

Mkuu wa mpango wa TB katika WHO Tereza Kasaeva amewaambia waandishi wa habari kuwa “ Haikubaliki kwamba  katika karne hii ya 21 watu mamilioni wapoteze maisha yao kutokana na magonjwa ambayo sio tu yanazuilika lakini pia kutibiwa”

 

Kifaa kinachotumiwa kwa chanjo dhidi ya kifua kikuu TB.Chanjo inatayarishwa  katika kituo cha afya Bougouni, Mali 2018.
© UNICEF/Ilvy Njiokiktjien
Kifaa kinachotumiwa kwa chanjo dhidi ya kifua kikuu TB.Chanjo inatayarishwa katika kituo cha afya Bougouni, Mali 2018.

 

Ameongeza kuwa kifua kikuu ni ugonjwa tegemezi kwa jamii na unahitaji hatua mtambukakukabiliana nao akisema kuwa  “Ni ugonjwa wa umaskini na bila kufikia watu maskini , bila kutoa hali muhimu kimaisha bila kutatua tatizo la utapiamlo ugonjwa huu haungeweza kutokomezwa.”

WHO inasema ili kuweza kufikia lengo la kutokomeza TB ifikapo mwaka wa 2030, mataifa yanahitaji kuharakisha mbinu za kuelekea mkabiliano na ugonjwa huo hususan  ufadhili wa ndani na nje.

Ripoti ya WHO inatoa taswira  ya ugonjwa huo na pia changamoto na vilevile nafasi vinavyokabili mataifa  katika jukumu la kukabiliana na ugonjwa huo.

Kwa ujumla vifo kutokana na kifua kikuu vimepungua mwaka jana ambapo mwaka 2017 kulitokea vifo  milioni 1.6 vikijumuisha vifo 300,000 vya watu wenye virusi vya Ukimwi. 

Ripoti inasema  tangu mwaka wa 2000 idadi ya watu wenye Ukimwi wanaofariki dunia kutokana na TB  imepungua kwa asilimia 44 ikilinganishwa na asilimia 29 kwa watu wasio na Ukimwi.

 

Mtot apewa chanjo dhidi ya kifua kikuu TB mjini Phnom Pehn, Cambodia
© UNICEF/Fani Llaurado
Mtot apewa chanjo dhidi ya kifua kikuu TB mjini Phnom Pehn, Cambodia

 

Ripoti inaongeza kuwa  mwaka 2017 duniani kote,   watu takriban  milioni 10,  waliugua  kifua kikuu.

Idadi ya maambukizi mapya inazidi kupungua kwa asilimia 2 kila mwaka, ingawa  kasi ya upunguaji kwa Ulaya ni asilimia 5 kila mwaka na Afrika asilimia 4 kila mwaka kati ya mwaka wa 2013 na 2017.

 Ripoti inasema pia kuwa kuna wasiwasi wa kuwepo kwa aina ya  kifua kikuu ambacho ni sugu kwa dawa.

Mwaka jana 2017 watu 558,000 walikadiriwa kupata usugu kwa dawa aina ya rifampicin, moja yadawa madhubuti ya kutibu kifua kikuu.

 Ripoti inatoa wito kuhamasisha kujitolea katika pande za kitaifa na kimataifa na kuhimiza viongozi wa nchi na serikali ambao watakutana wiki ijayo kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa wa hali ya juu kuhusu kifua kikuu, wachukue hatua madhubuti.