UNGA73 yaanza rasmi, rais wake asema mabadiliko ya tabianchi hayakomi ijumaa

17 Septemba 2018

Rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulioanza rasmi hii leo Maria Fernanda Espinosa ametaja mambo muhimu yatakayoongoza utendaji wake kwa kipindi kizima cha mwaka mmoja.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa Bi. Espinosa ambaye ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ecuador ametaja mambo hayo kuwa ni Tekeleza, Uwajibikaji, Husisha na Ufanisi ambayo kwa kiingereza kifupi chake ni DARE, D.A.R.E inamaanisha "Tekeleza, wajibika, husisha, ufanisi. Kwa hivyo, kuhuisha na kuimarisha ushirikiano wa mataifa, kuhuisha Baraza Kuu, Kuhuisha mfumo wa Umoja wa Mataifa. Sote tunahitaji na sisi sote tutanufaika na mfumo wa kimataifa wenye kanuni thabiti..”

Bi. Espinosa akasema kwamba amejiwekea vipaumbele saba kwa kuwa  "kwa  sababu tunahitaji kufanya kazi siku saba kwa wiki. Tunahitaji kufanya kazi kwa ajili ya watu walio na shida, masikini, wakimbizi, siku saba kwa wiki. Mabadiliko ya tabia nchi hayakomi Ijumaa.”

Rais wa Baraza Kuu la UN UN Photo/Manuel Elias akiwa na Monica Grayley kutoka UN News
UN News
Rais wa Baraza Kuu la UN UN Photo/Manuel Elias akiwa na Monica Grayley kutoka UN News

Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alipoulizwa ni kwa jinsi gani anaona dhima ya nafasi hiyo akasema hivi sasa imebadilika ikilinganishwa na miaka ya 80 na 90 ambapo ilikuwa ni ya kiitifaki zaidi. “rais ambaye angekuja New York na kuongoza kazi za Baraza Kuu wakati wa kikao, kuanzia Septemba, mpaka Disemba, lakini sasa ni nafasi ya kisiasa yenye wajibu mkubwa, kuongoza kweli kazi za Baraza Kuu kwa mwaka mzima.”

Na alipoulizwa kuhusu anajisikia vipi kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo kutoka nchi za Amerika ya Kusini, Bi. Espinosa amesema ni heshima lakini pia ni changamoto kubwa  "kwa sababu sisi wanawake, tunapokuwa katika nafasi za mamlaka au nafasi zilizo na wajibu wa juu, tunapaswa kufanya kazi mara mbili. Tunapaswa kufanya mara mbili, kwa sababu matarajio ni ya juu. Na ninadhani kuwa katika ulimwengu ambao bado unaendeshwa na wanaume, ni changamoto kubwa kwa sababu unatakiwa kuuthibitishia ulimwengu kuwa una uwezo, kwamba unaweza kutekeleza wajibu wako.”

Bi. Espinosa ameanza rasmi kuongoza mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baada ya mkutano wa 72 uliokuwa ukiongozwa na Miroslav Lajčák kukunja jamvi hii leo. K wa mujibu wa taratibu za makabidhiano,  Bwana Lajčák alihutubia Baraza kufunga mkutano wake akifuatiwa na Katibu Mkuu Antonio Guterres ambapo hatimaye Bi. Espinosa alipatiwa nyundo ya kuongoza kikao na kukaribisha wajumbe na baadaye alizungumza na waandishi wa habari.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Bi. Espinosa amesema " nitashirikiana na nchi zote wanachama kusongesha mbele ajenda ya Umoja wa Mataifa na kuhakikisha sauti za pande zote ikiwemo za raia wa kawaida, wanawake na watoto wanaokandamizi zinajumuishwa,."

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter