Mwanamke kuongoza Baraza Kuu la UN, ni baada ya zaidi ya muongo mmoja

5 Juni 2018

Baada ya miaka 12, mwanamke achaguliwa tena kuwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limemchagua Maria Fernanda Espinosa wa Ecuador kuwa rais wa Mkutano wa 73 wa baraza hilo, UNGA73.

Uchaguzi huo umefanyika leo ambapo Bi. Espinosa amepata kura 128 huku mpinzani wake Mary Elizabeth Flores Flake kutoka Honduras ambaye amepata kura 64.

Rais mteule huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa atachukua nafasi inayoachwa na Miroslav Lajčák  ambaye anahitimisha urais wa mkutano wa 72 wa baraza hilo mwezi Septemba.

Akizungumza baada ya uteuzi, Bi. Espinosa amesema, “nitasongesha masuala ya ushirikiano wa kimataifa ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.”

Maria Fernanda Espinosa

Naye Bwana Lajčák  ambaye atamkabidhi rasmi kijiti cha urais wa Baraza hilo Bi. Espinosa mwezi Septemba mwaka huu, amezungumza baada ya kutangaza matokeo ya uchaguzi huo akisema..

Miroslav Lajčák 

“Anakuwa mwanamke wa nne kushika wadhifa huu katika historia ya Umoja wa Mataifa. Kusema kweli, wanawake wanne kati ya marais 73 wa baraza si rekodi ya kujivunia. Lakini nina furaha kuwa tunasonga mbele. Miezi michache ijayo itakuwa muhimu, kwa kuwa maandalizi ya mkutano wa 73 yanaanza.”

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametumia fursa ya mkutano huo kumpongeza Bwana Lajčák  ambaye anamaliza muda wake akisema kuwa amehudumu katika kipindi muhimu cha kuleta mabadiliko ya mfumo wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa.

María Fernanda Espinosa Garcés, Rais mteule wa Baraza Kuu la UN akihutubia wajumbe baada ya kuchaguliwa kuongoza kikao cha 73 cha baraza hilo. Yeye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Ecuador.
UN /Loey Felipe
María Fernanda Espinosa Garcés, Rais mteule wa Baraza Kuu la UN akihutubia wajumbe baada ya kuchaguliwa kuongoza kikao cha 73 cha baraza hilo. Yeye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Ecuador.

“Hii imekuwa kipindi cha mkutano muhimu, ukipatiwa umuhimu zaidi na hatua ya kihistoria ya wiki iliyopita ya kupitishwa kwa azimio la kufanyia marekebisho na kujipanga upya kwa mfumo wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa,” amesema Katibu Mkuu.

Na ndipo akatoa pongezi pia kwa Bi. Espinosa akisema kuwa..

Antonio Guterres

“Naamini, kama alivyosema rais, tunaweza na tunapaswa kufanya vyema zaidi kuliko rekodi ya sasa ya wanawake wanne kati ya 73 kushika wadhifa wa urais wa baraza kuu, ambapo wawili walifanya hivyo nusu karne iliyopita. Hakuna mwanamke hata mmoja kutoka barani mwangu iwe Ulaya Magharibi au Ulaya Mashariki. Hebu na uchaguzi wa leo ufungue njia ya kusongesha maendeleo kuelekea usawa wa kijinsia ndani na nje ya Umoja wa Mataifa.”

Bi. Espinosa ambaye sasa ni Waziri wa mambo nje wa Ecuador ameshika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya nchi hiyo kama waziri wa ulinzi na usalama na pia mwakilishi wa kudumu wa Ecuador katika Umoja wa  Mataifa mjini New York, Marekani na pia Geneva, Uswisi.

Taaluma yake ni mwanasayansi aliyesomea masuala ya misitu, masuala ya kijami, siasa na elimu ya mambo ya kale.

Licha ya siasa Bi Espinosa pia ni mwandishi wa vitabu, ngonjera na insha katika vyuo vikuu nchini Ecuador.

Wengine waliowahi kushika wadhifa huo ni Vijaya Lakshimi Pandi wa India mwaka 1953, Angie Elizabeth Brooks wa Liberia mwaka 1969 na Sheikha Haya Rashed Al Khalifa wa Bahrain mwaka 2006.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter