Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Palestina inaongoza kwa ukosefu wa ajira duniani:UNCTAD

Hospitali ya Ash Shifa mjini Gaza
OCHA
Hospitali ya Ash Shifa mjini Gaza

Palestina inaongoza kwa ukosefu wa ajira duniani:UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Kiwango cha ukosefu wa ajira katika eneo linalokaliwa la Wapalestina ndicho kinachoongoza duniani kikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 27, pato la kila mtu likishuka, uzalishaji wa kilimo ukipungua kwa asilimia 11 na huku hali ya kiuchumi na kijmii kwa mwaka 2017 ikizorota zaidi.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya msaada kwa watu wa Palestina iliyotolewa leo na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo na biashara UNCTAD .

Ripoti pia inaeleza kwamba masharti yaliyowekwa na utawala wa Israel katika eneo hilo yanawaathiri vibaya wanawake na vijana, na kuonya kwamba kupungua kwa msaada wa ufadhili, kusitishwa kwa ujenzi mpya wa Gaza na kutokuwepo na mikopo endelevu ya fedha kwa umma kunaweka njia panda mustakabali wa sekta za umma na binafsi Palestina.

Matarajio ya uchumi wa Gaza yanafifia zaidi kutokana na vita vinavyoendelea lakini pia kuponkonywa ardhi zao na maliasili na taifa linalowakalia.

Kwa mujibu wa mratibu msaidizi wa UNCTAD kitengo cha watu wa Palestina Mahmoud Elkhafif “chini ya sheria za kimataifa, Israel, na jumuiya ya kimataifa wanawajibu sio tu wa kuepuka hatua ambazo zitadumaza maendeleo lakini pia kuchukua hatua madhubuti kuchagiza maendeleo katika eneo linalokaliwa laWapalestina.” Ameongeza kuwa “hata hivyo Israel imeshindwa kulegeza vikwazo na msaada kutoka kwa wafadhili umepungua sana na kufikia theluthi moja 2018.”

Vikwazo vingi Ukingo wa Magharibi na upanuzi wa makazi haramu ya Walowezi

Mwaka 2017 na mapema mwaka huu 2018 ujenzi wa makazi mapya ya Walowezi uliongezeka licha ya azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Desemba 2017 ambao Baraza hilo “lilisisitiza kwamba maamuzi yoyote na vitendo vyovyote ambavyo vinabadili tabia, hali au idadi ya watu katika mji mtakatifu wa Jerusalemu hayana athari za kisheria, lakini si halali, haipaswi na ni lazima zizingatie maazimio husika ya Baraza la Usalama”.

 

Mali ya Palestina yabomolewa eneo la ukiongo wa magharibi mwaka 2016
Photo: OCHA
Mali ya Palestina yabomolewa eneo la ukiongo wa magharibi mwaka 2016

 

Ripoti ya UNCTAD inaainisha ushahidi wa upokonyaji wa sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi ikiwa ni pamoja na kuwahamishia watu wa Israeli katika makazi mapya, kulazimisha watu wa Palestina kuhama , uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 19 katika ujenzi wa makazi ya Walowezi, kupanua mamlaka ya kisheria ya ndani ya Israeli kwa Walowezi na kutekeleza hatua za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutawala ambazo zinazidisha ujumuishaji wa makazi hayo katika mfumo wa Serikali ya Israeli.

Vikwazo kwa zaidi ya muongo vyazidi kudumaza maendeleo Gaza

Wakati vikwazo na vizuizi vya Israel vikiingia mwaka wa 11 sasa, Ukanda wa Gaza umegeuka kuwa janga la kibinadamu lililoghubikwa na madhila na utegemezi wa misaada kila uchao imesema ripoti hiyo.

Uwezo wa uzalishaji Gaza umelemazwa na operesheni kubwa tatu za kijeshi na vikwazo vya anga, baharini na nchi kavu.

Mwaka 2008-2009 operesheni za kijeshi za Israel zilifuta zaidi ya asilimi 60 ya mtaji wa jumla wa akiba ya uzalishaji Gaza na mashambulizi ya 2014 yalisambaratisha asilimia 85 ya kile kilichosaliaSamani zilizosambaratishwa ni pamoja na barabara, vituo vya nishati, viwanda na majengo ya biashara, ardhi za kilimo na pia miundombinu mingine.

 

Taka zilizorundikana katika eneo la Ash Sheikh Radwan mjini Gaza. Chakula nacho ni taabu  kupatikana
OCHA
Taka zilizorundikana katika eneo la Ash Sheikh Radwan mjini Gaza. Chakula nacho ni taabu kupatikana

 

Mwaka 2012 Umoja wa Mataifa ulionya kwamba mwenendo unaoendelea usipobadilika Gaza haitokalika tena, haitofaa kwa wanadamu kuishi ifikapo 2020.

Na tangu hapo ripoti inasema , viashiria vyote vya maendeleo ya kiuchumi na kijamii vimezidi kudorora na hali Gaza imetoka kuwa mbaya na sasa ni zahma kubwa.

Juhudi za nusuru hali hilo zimejikita zaidi katika misaada ya kibinadamu imesema ripoti, na hii inaacha rasilimali ndogo sana kwa ajili ya maendeleo na kufufua shughuli za kiuchumi. Hivi sasa Gaza uchumi kwa mtu uko asilimia 30 chini ya ilivyokuwa mwanzo wa karne hii. Umasikini na kutokuwepo uhakika wa chakula vimetapakaa ingawa asilimia 80 ya watu wanapata msaada wa huduma za hifadhi ya jamii.

Gaza pia imekuwa na tatizo kubwa la umeme ambalo linaongezeka  mapema mwaka huu 2018 wakati wanapata huduma ya umeme kwa saa mbili tu kwa siku huku tatizo hilo likiendelea kuathiri maisha ya kila siku ikiwemo shuguli za uzalishaji na utoaji wa huduma muhimu za msingi kwa jamii.

 

Baraza lataka uchunguzi kuhusu kilichotokea Gaza
Picha ya OCHA oPt
Baraza lataka uchunguzi kuhusu kilichotokea Gaza

 

Cha kufanya kuwanusuru watu wa Palestina

Kupitia madhila yote hayo ya kukosa huduma za msingi za kiuchumi, kijamii na haki za binadamu kuifanya Gaza na watu wake kuathirika kijamii na kisaikolojia , kukitajwa kuwa na kiwango kikubwa cha watu wenye msongo wa mawazo na wanaojiua.

Kwa mfano mwaka 2017 ripoti inasema watoto 225,000 au zaidi ya asilimia 10 ya watu wote walihitaji msaada wa kisaikolojia.

Ilikuhakikisha kunakuwa na ujenzi endelevu wakuikwamua Gaza ni lazima kuondoa kabisa vizuizi na vikwazo vya Israel, kuunganisha tena Gaza na Ukingo wa Magharibi kiuchumi na kukomesha tatizo la umeme haraka iwezekanavyo, lakini pia kuiwezesha mamlaka ya mapato ya Palestina kuanzisha maeneo ya kuchimba gesi kwenye baharí ya Mediterranea , ambayo iligunduliwa kuwepo katika miaka ya 1990.

Jinamizi katika biashara ya Wapalestina

Vikwazo vya Israel kwa biashara ya Palestina ni pamoja na kutoruhusu Wapalestina kuingiza kutokanje bidhaa mbalimbali za raia ambazo zinauwezekano wa kutumika kijeshi kwa mujibu wa ripoti.

Orodha ya bidhaa hizo ni pamoja na mashine mbalimbali, vipuri, mbolea, kemikali, vifaa vya matibabu, vifaa vya mawasiliano, chuma, mabomba ya chuma, mashine za kusaga, vifaa vya macho na vifaa vya usafiri.

Nyumba ya familia ya Palestina katika ukanda wa Gaza ilibomolewa na watawala wa Israel
Photo/UNRWA
Nyumba ya familia ya Palestina katika ukanda wa Gaza ilibomolewa na watawala wa Israel

 

Kupiga marufuku kwa bidhaa hizo kuna gharama kubwa za kiuchumi na kunachochea hali ya vita na kutokuwepo kwa utulivu wa kisiasa kwa kudhoofisha ajira, mishahara na maisha ya watu wa Palestina.

Kuondoa vikwazo vya Israeli kwa biashara ya Palestina na uwekezaji vinaweza kuruhusu uchumi wa eneo hilo kukua kwa asilimia 10, wakati hali hiyo inaweza kuhakikisha tu kuendelea kwa ukosefu wa ajira ya kiwango cha msongo wa mawazo na umasikini uliokithiri, imeonya ripoti hiyo.