Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lesotho, Afrika Kusini, Bahrain na India kidedea kuvutia  uwekezaji

Mashine za kufua umeme kwa upepo
UN Photo/Eskinder Debebe)
Mashine za kufua umeme kwa upepo

Lesotho, Afrika Kusini, Bahrain na India kidedea kuvutia  uwekezaji

Ukuaji wa Kiuchumi

Jukwaa la kimataifa la uwekezaji likiwa limeanza leo huko Geneva, Uswisi, mamlaka nne za uwekezaji, IPA kutoka Bahrain, India, Lesotho na Afrika Kusini zimeibuka washindi kutokana na mchango wao katika kuvutia uwekezaji katika nchi zao.

Mamlaka hizo zimeshinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya uendelezaji uwekezaji, kwa kuzingatia kuwa uwekezaji wao unachochea faida za kiuchumi na kijamii na hivyo kusaidia nchi zao kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Tuzo hizo zilizoandaliwa na kamati ya maendeleo na biashara ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD zinalenga kutambua mamlaka za uwekezaji, IPAs, katika nchi husika pamoja na serikali na pia kuonyesha mifano bora ya kuvutia uwekezaji unaopatia kipaumbele SDGs.

Akizungumzia mamlaka hizo, Mkurugenzi wa uwekezaji wa UNCTAD James Zhan amesema kampuni hizo zilizoshinda zimedhihirisha kuwa kwa kujumuisha SDGS, mamlaka za uwekezaji zinaweza kuwa na mchango bora kwenye maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mamlaka zilizoibuka kidedea ni ile ya maendeleo ya kiuchumi Bahrain, EDB ambayo kwa mujibu wa majaji wa shindano hilo ilitoa huduma ya kanzi data kupitia kompyuta kadhaa ndani na nje ya Bahrain na hivyo kusaidia kueneza elimu ya teknolojia kwenye eneo la Mashariki ya Kati.

Kutoka India, mamlaka ya uwekezaji ikipatiwa  jina Wekeza India ilipata tuzo kwa mchango wake kwenye kusaidia kampuni  moja kubwa ya tabo za upepo duniani kuanzisha  mtambo wa kuzalisha bapa za viwandani huku ikiazimia kupatia wafanyakazi stadi za kuzalisha nishati endelevu.

Nalo shirika la taifa la mandeleo Lesotho, LNDC limeibuka kidedea kwa uwekezaji wake kwenye mradi mkubwa wa kilimo cha mboga mboga na matunda ambacho kitaanzisha ajira 15,000.

Kutoka Afrika Kusini, UNCTAD imeipatia tuzo mamlaka ya uwekezaji nchini humo, Wekeza Afrika Kusini kwa kuwezesha kuanzishwa kwa miradi ya kubadilisha taka kuwa lishe kwa Wanyama.

Jukwaa hilo linahudhuriwa pia na marais 14 wakiwemo kutoka Armenia, Bangladesh, Botswana, Cambodia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kenya, Lesotho, Malawi, Mongolia, Montenegro, Namibia, Sierra Leone na USwisi.