Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye hukumu dhidi ya wahalifu wa Hotel ya Terrain, Sudani Kusini, yatolewa

Wakimbizi wa ndani kutoka vituo vya kuwalinda raia (PoC site) mjini Juba, wakijificha kutokana na mapigano kati ya SPLA na SPLA-IO.
UN Photo/Eric Kanalstein
Wakimbizi wa ndani kutoka vituo vya kuwalinda raia (PoC site) mjini Juba, wakijificha kutokana na mapigano kati ya SPLA na SPLA-IO.

Hatimaye hukumu dhidi ya wahalifu wa Hotel ya Terrain, Sudani Kusini, yatolewa

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Uchunguzi wa mahakama ya kijeshi  dhidi ya waliotekeleza uhalifu baada ya kushambulia  Hotel ya Terrain mjini Juba nchini Sudan Kusini , umekamilika na hukumu kutolewa hii leo.

Askari 10 wa jeshi la Sudan Kusini wamekutwa na hatia ya kufanya uhalifu dhidi ya raia, hatua ambayo hatimaye imetoa haki kwa waathirika na familia ya mwandishi wa habari ayeuawa katika shambulio hilo.

Majaji wamewasilisha uamuzi wao leo na kuwapa askari hao adhabu ya kifungo cha muda mrefu gerezani kwa makosa ya  mauaji, ubakaji na makosa mengine. Mahakama pia imeamuru serikali kulipa fidia kwa waathirika.

Waathirika na manusura wa shambulio hili la kutisha la Julai 2016 walistahili haki na baada ya muda mrefu , leo. Hata hivyo, kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa wakati wa kesi hiyo, maswali yanabakia kuhusu iwapo uwajibikaji kwa uhalifu huu umefikia ngazi zote za juu za amri.

Ingawa hukumu hii haitaondoa maumivu, hasara na mateso yaliyosababishwa na matendo mabaya ya vurugu yaliyofanywa na wahalifu hawa, ni muhimu kwamba hatimaye wahalifu hao wamewajibishwa wazi wazi na sharia imechukua mkondo wake. Matokeo ya hukumu hii pia yanatuma ujumbe wenye nguvu kwa wahalifu wengine pamoja na wanajeshi, kwamba watahukumiwa na kuadhibiwa kwa matendo yao.

Mashahidi na manusura walionyesha ujasiri na uvumilivu kwa kushiriki katika mchakato wa mahakama ulioanza mwezi Mei 2017.

Kulikuwa na changamoto kubwa katika mchakato huo, ikiwa ni pamoja na hali ya watuhumiwa kizuizini, vikwazo vingine vya upatikanaji wa washauri kwa watuhumiwa, na changamoto nyingine ilikuwa kesi ya uhalifu huu dhidi ya raia kufanyika katika mahakama ya kijeshi badala ya mahakama ya kiraia

Hata hivyo, kesi ilivyoendelea, kulikuwa na utayari wa kupokea utaratibu mpya ikiwa ni pamoja na kuruhusu ambao hawawezi au hawataki kuhudhuria wao wenyewe kutoa ushuhuda kupitia video na pia kutumia mahakama za ndani ili kuzuia jamii kuwatambua waathirika.

Mashitaka haya yaliwaleta mbele ya mkono wa sheria wahalifu walioshiriki katika tukio mahususi la Hoteli ya Terrain ambapo wafanyakazi wa kimataifa walitengwa. Hata hivyo, bado kuna tatizo kubwa la unyanyasaji kingono na kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wa Sudani Kusini. Matukio mengi huenda yanapita bila kuripotiwa na hivyo bado kuna ukatili.

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani Sudan Kusini- UNMISS una nia ya kufanya kazi na mamlaka nchini Sudan Kusini kushughulikia baadhi ya changamoto zilizotajwa wakati wa hukumu hii na pia kuunga mkono jitihada za kuboresha uhuru na ufanisi wa mfumo wa haki ili waathirika wengi wa unyanyasaji wa kingono na vurugu nyingine waweze kupata haki yao mahakamani.