Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yawasweka rumande  walinda amani 46 Sudan Kusini

Walinda amani katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS. Picha: UM/JC McIlwaine

UNMISS yawasweka rumande  walinda amani 46 Sudan Kusini

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) umewachukulia hatua ya kinidhamu askari walinda amani wa Umoja wa Mataifa 46 wanaotuhumiwa kujihusisha katika vitendo vya unyanyasaji wa kingono katika mji wa Wau Sudan kusini.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya uchukunguzi wa taarifa zilizofikishwa katika ofisi ya UNMISS mnamo  tarehe 8 Februari kuhusu tuhuma inayowakabili askari walinda amani kutoka Ghana (FPU) kuhusu vitendo vya unyanyasaji wa kingono kwa wanawake  wakimbizi wa ndani wanaoishi katika kambi iliyopo chini ya ulizni wa Umoja wa Mataifa huko Wau.

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo David Shearer pamoja na ofisi huru juu ya uchunguzi ya Umoja wa mataifa OIOS, waliwasilisha ripoti ya  uchunguzi wa awali mnamo tarehe 22 Februari, na siku  hiyo hiyo mchana, UNMISS ikachukua uamuzi wa kuwaondoa mara moja askari hao kutoka kwenye vituo vyao vya kazi katika mji wa  Wau ambapo kitengo cha askari hao, kilihamishiwa Juba kwa siku mbili zilizofuata na asakari  46 walitiwa nguvuni katika mji mkuu wa Sudan Kusini.

UNMISS imesema imechukua hatua ya  haraka ili  kulinda na pia kusaidia waathirika na mashahidi katika kesi hii wakati uchunguzi kamili unaendelea ili kubaini watuhumiwa  na kuwafikisha mbele ya haki.