Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya Umoja wa Mataifa yaiamuru Uganda kuilipa DR Congo dola milioni 325

Muonekano wa Jumba la Amani, makao ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague, Uholanzi, 2005
ICJ/Jeroen Bouman
Muonekano wa Jumba la Amani, makao ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague, Uholanzi, 2005

Mahakama ya Umoja wa Mataifa yaiamuru Uganda kuilipa DR Congo dola milioni 325

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mahakama ya Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya haki, ICJ imeitaka Uganda kuilipa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dola milioni 325 kama fidia kuhusiana na mzozo wa kikatili kati ya mataifa hayo mawili kuanzia 1998 hadi 2003.

Ikitoa uamuzi wake, Mahakama ya ICJ imegawanya kiasi hicho cha fedha kama ifuatavyo:-

  1. DRC itapatiwa dola milioni 225 kwa uharibifu kwa watu, ambayo ni pamoja na watu kupoteza maisha, kubakwa, kuajiri watoto askari na baadhi ya raia kufurushwa.
  2. Nchi hiyo pia itapokea dola milioni 40 kwa uharibifu wa mali.
  3. Na dola milioni 60 kwa uharibifu wa maliasili, ikiwa ni pamoja na uporaji wa dhahabu, almasi na mbao.

Fidia inaonesha madhila yaliyopatikana

Rais wa ICJ Jaji Joan Donoghue amesema “Mahakama  inabainisha kuwa malipo yaliyotolewa kwa DRC kwa uharibifu wa watu na mali yanaonesha madhara waliyopata watu binafsi na jumuiya kutokana na ukiukwaji wa wajibu wa kimataifa ya Uganda.”

Awali DRC iliwasilisha kesi hiyo kwa ICJ mwezi Juni 1999, ikitaja vitendo vya uvamizi wa kutumia silaha vilivyofanywa na Uganda katika eneo lake la mamlaka kuwa ni "Ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa pamoja na Mkataba wa Umoja wa Afrika.”

Katika kilele cha vita, zaidi ya nchi tisa za Kiafrika zilishiriki kutafuta suluhu kwenye mapigano.
Mahakama iliamua Desemba 2005 kwamba Uganda ilipaswa kulipa fidia kwa DRC, lakini pande zote hazikuweza kufikia makubaliano.
Uganda imeagizwa kulipa dola milioni 325 kwa awamu tano za kila mwaka za dola milioni 65, kuanzia Septemba.

ICJ Mahakama ya Dunia

ICJ, pia inajulikana kama "Mahakama ya Dunia", ni chombo cha juu zaidi cha mahakama cha Umoja wa Mataifa.

Mahakama hii hutatua mizozo ya kisheria iliyowasilishwa kwake na Mataifa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Pia inatoa maoni ya ushauri kuhusu maswali ya kisheria yanayorejelewa na vyombo vya Umoja wa Mataifa vilivyoidhinishwa na mashirika maalumu.

  • Hukumu katika mizozo kati ya Mataifa ni lazima itekelezwe.
  • ICJ inaundwa na majaji 15 na iko mjini The Hague nchini Uholanzi.