Malawi chunguzeni vitisho dhidi ya watetezi wa haki za binadamu :OHCHR
Udhalilishaji pamoja na vitisho wanavyokabiliana navyo watetezi wa amani nchini Malawi yafaa kuchunguzwa.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Geneva Uswisi na msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu OHCHR Liz Throssell.
Msemaji huyo ameongeza kuwa visa hivyo dhidi ya watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati nchini humo vimeongezeka ambapo visa kadhaa vimeripotiwa katika wiki chache zilizopita vikiwemo dhidi ya wanawake kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka ujao.
Ofisi ya haki za binadamu pia ina wasiwasi kutokana na mwelekeo unaojitokeza wa kutoa vitisho dhidi ya wabunge wanawake na pia wagombea wa viti mbalimbali.
Ofisi hiyo inatoa wito kwa serikali nchini Malawi kuhakikisha kwamba vitisho na hujuma dhidi ya watetezi wa haki za binadamu vinachunguzwa kikamilifu na pia kazi muhimu za wafanyakazi wa asasi za kiraia zinalindwa kwa mujibu wa sheria za haki za binadamu za kimataifa.
Ofisi ya haki za binadami imesisitiza kuwa ni lazima kuweka mazingira bora kabla ya uchaguzi mkuu ili kila mtu aweze kutumia kikamilifu haki ya kujieleza, kukusanyika kwa amani na haki ya kujumuika.