Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya Nicaragua heshimuni haki ya watu kukusanyika: UN

Waandamanaji wakitaka kukomeshwa kwa ukatili Nicaragua
Artículo 66
Waandamanaji wakitaka kukomeshwa kwa ukatili Nicaragua

Serikali ya Nicaragua heshimuni haki ya watu kukusanyika: UN

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imetoa wito kwa viongozi wa serikali ya Nicaragua kuheshimu haki ya kutoa maoni na kujieleza kwa uhuru na pia kukusanyika. 

Taarifa hii imetolewa hii leo katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi na msemaji wa ofisi ya OHCRC Liz Throssell baada ya ripoti kueleza kuwa mamlaka nchini humo zinaendelea kuyafanya matendo halali ya viongozi wa kiraia kuwa ni ya kijinai na mengine yakihusishwa na migomo na maandamano yaliyolipuka katika nchi hiyo mwanzoni mwa mwaka huu.

Taarifa imesema wakati katika miezi ya hivi karibuni maandamano yamepungua kwa kiasi kikubwa nchini Nicaragua bado nchi haionekani kurejea katika hali ya kawaida, “tunahofia kuwa mamlaka zimewadhibiti watu wasishiriki katika maandamano na kimabavu kuwazuia watu kutimiza haki yao ya kuandamana”.

Msemaji huyo ameeleza pia kuwa kulingana na takwimu za serikali ya Nicaragua, watu 273 wanashikiliwa wakihusishwa na maandamano ya tarehe 5 mwezi huu lakini mashirika yasiyo ya kiserikali yanasema wanaoshikiliwa wanakadiriwa kufikia 586.

Pia Bi Throssell amesema OHCHR imepokea ripoti kuwa hukumu za haki hazizingatiwi katika kesi dhidi ya wakulima na viongozi wa wanafunzi  waliohusika katika maandamano. Msemaji huyo ameongeza kuwa OHCHR inaendeleaa kufuatilia hali ya haki za binadamu nchini Nicaragua na kiutoa ripoti kila mwezi kuhusiana na hali hiyo.

Mwanafunzi wa udaktari mwenye umri wa miaka 21 akionesha kovu alilolipata kutokana na machafuko nchini Nicaragua
UNHCR/Roberto Carlos Sanchez
Mwanafunzi wa udaktari mwenye umri wa miaka 21 akionesha kovu alilolipata kutokana na machafuko nchini Nicaragua

 

Mwezi Mei mwaka huu, OHCHR iliiomba kibali kwa serikali ya Nicaragua ili iweze kuingia nchini humo kwa ajili ya kukusanya taarifa kuhusu kile kilichotokea wakati wa maandamano na pia kuchukua hatua za kusaidia kuzuia hali kama hiyo ya ukiukwaji wa haki za binadamu kutokea tena.

“Tunarudia tena kueleza kuwa tuko tayari kuisaidia serikali katika kufikia jukumu lao la kutunza haki za kimataifa za binadamu” amesema Bi. Throssell.