Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokomeza nyuklia ni kuachana nazo kabisa- Guterres

Wauatiliaji wasilaha za nyuklia URENCO Netherlands.
IAEA/Dean Calma
Wauatiliaji wasilaha za nyuklia URENCO Netherlands.

Kutokomeza nyuklia ni kuachana nazo kabisa- Guterres

Amani na Usalama

Njia pekee ya kutokomeza tishio la silaha za nyuklia duniani ni kuachana kabisa na silaha hizo, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akihutubia mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kando mwa mjadala mkuu wa  baraza hilo jijini New York, Marekani.

Mkutano huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza silaha za nyuklia ambapo Katibu Mkuu amesema kinachotia hofu hata hivyo ni kasi ya mashindano ya umiliki wa silaha hizo.

Amesema ingawa suala la kutokomeza silaha za nyuklia limekuwa kipaumbele cha Umoja wa Mataifa tangu kuanzishwa kwake baada ya vita vikuu vya pili vya dunia, “cha kusikitisha, si kwamba harakati za kutokomeza nyuklia zimekoma, bali zimegeuka na sasa ni kasi ya kutengeneza. Uhusiano kati ya serikali zinazomiliki nyuklia nao umezingirwa na ukosefu wa kutoaminiana. Kauli za hatari kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia zinaongezeka.”

Katibu Mkuu amesema “tunahaha kuwa na dunia isiyo na nyuklia kwa sababu tunafahamu vyema hatari zake na uwezekano wake wa kutokomeza uwepo wa sayari yetu,” akiongeza kwamba “tunafahamu kuwa matumizi yoyote ya silaha za nyuklia yanaweza kuwa janga la kibinadamu.”

Katibu Mkuu amesema zaidi ya yote kuna mgawanyiko mkubwa hivi sasa kuhusu kasi na kiwango cha kudhibiti kuenea kwa nyuklia na kwamba wasiwasi wake ni kuwa “Tunarejea kwenye tabia mbaya ambazo kwa mara nyingine tena zinaweza kuteka dunia yetu kuwa katika mwelekeo wa kutokomeza nyuklia.”

Amekumbusha kuwa kufuatia kumalizika kwa muda wa mkataba wa kipekee wa kimataifa wa kudhibiti nyuklia, INF, dunia hivi sasa imepoteza kidhibiti kikuu cha vita vya nyuklia.

Kwa mantiki hiyo amesihi Marekani na Urusi ziongeze muda wa kile kinachoitwa mwanzo wa mkataba mpya ili kuweka utulivu na muda zaidi wa mashauriano juu ya jinsi ya kudhibiti matumizi ya silaha hizo.

Halikadhalika ametoa wito kwa nchi wanachama kushirikiana katika tathmini yam waka 2020 ya mkataba wa kudhibiti kuenea kwa nyuklia, NPT ili kuhakikisha mkataba huo unasalia na uwezo wa kukidhi malengo yake ya msingi ya kuzuia vita vya nyuklia na kuwezesha utokomezaji wa silaha hizo.