Tushikamane na DRC ili mchakato wa uchaguzi umalizike kwa amani -MONUSCO

11 Januari 2019

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha kawaida kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambapo wajumbe wamepata taarifa kuhusu kinachoendelea hivi sasa nchini humo kufuatia kutangazwa kwa Felix Tshisekedi kuwa rais mteule wa  nchi hiyo. 

Leila Zerrougui, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC akihutubia kwa njia ya video kutoka mjini Kinshasa amesema tangazo hilo la matokeo lilipokewa kwa mtazamo tofauti ambapo mshindi alisema atakuwa raisi wa wote ilhali ushirika wa upinzani ulipinga matokeo hayo na kuchochea ukosefu wa utulivu.

Ametaja maeneo kama jimbo la Kwilu ambapo ghasia zilisababisha watu wapatao 12 kuuawa wakiwemo polisi na raia huku mali zikiharibiwa.

Amesema hivi sasa wanajiandaa kupeleka watu wao huko Kikwit kutathmini hali halisi na kuzuia ghasia kwa kuwa eneo hilo hakuna walinda amani wa ujumbe wa  Umoja wa Mataifa MONUSCO.

Taswira ya tarehe 30 Desemba 2019 wakati wananchi wa DRC walipopiga kura kuchagua rais na wabunge na viongozi wa majimbo.
MONUSCO/Alain Likota
Taswira ya tarehe 30 Desemba 2019 wakati wananchi wa DRC walipopiga kura kuchagua rais na wabunge na viongozi wa majimbo.

Huko Kisangani na maeneo ya jimbo la Kasai matukio pia ya ghasia yaliripotiwa na wanachunguza taarifa za vifo.

Bi. Zerrougui ambaye pia ni mkuu wa MONUSCO amelaani ghasia hizo na kutoa rai kwa wananchi kuepuka vitendo vya ghasia na kujizuia wakati huu.

Amewaambia wajumbe kuwa wiki zijazo zinaweza kughubikwa na michakato ya kupinga matokeo na mahakama ya kikatiba kutathmini matokeo.

Kwa mantiki ofisi  yake itaendelea kushirikiana na wadau wote nchini DRC ili kuhakikisha kuwa mchakato wa kihistoria unamalizika kwa amani.

Amesihi mshikamano na wana DRC wakati nchi hiyo inajiandaa kubadilisha mamlaka ya ngazi ya juu kwa amani.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter