Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yaomba msaada kwa wahamiaji waliotimuliwa katika migodi ya dhahabu, Chad

Mwanamke mmoja  akiwa anapita katika kijiji kimoja nchini Chad.(Kumbukumbu)
Naomi Frerotte
Mwanamke mmoja akiwa anapita katika kijiji kimoja nchini Chad.(Kumbukumbu)

IOM yaomba msaada kwa wahamiaji waliotimuliwa katika migodi ya dhahabu, Chad

Amani na Usalama

Shirika  la Uhamiaji la  Umoja wa Mataifa,  IOM linaomba jamii ya kimataifa liipatie dola zaidi ya 500,000 ili kutoa msaada wa kibinadamu au kurejesha nyumbani maelfu ya wahamiaji walioathiriwa na hatua ya serikali ya Chad, ya  kusitisha shughuli zote za uchimbaji huko Miski na Kouri Bougri, ambayo ni miongoni mwa machimbo makubwa zaidi ya dhahabu nchini  humo.

Serikali ilichukua uamuzi huo kufuatia shambulio dhidi ya kituo chake cha askari wa mpakani kilichopo karibu na machimbo hayo makubwa zaidi ya dhahabu katika eneo la Tibesti, tarehe 11  mwezi huu wa Agosti.

Machimbo haya yaliyopo karibu na mpaka  wa Chad na Libya yamekuwa yakivutia wafanyakazi wahamiaji kutoka Afrika ya Kati, Afrika Magharibi na ndani ya Chad tangu mwaka 2013.

Kufungwa  ghafla kwa machimbo haya kumesababisha wahamiaji hao kuhamia miji ya Zouarke na Zouar katika eneo la Tibesti, huku angalau watu 3,800 wakiwa wamehamia Faya katika eneo la Borkou kaskazini mwa Chad.

IOM imesema uhamiaji huo wa hivi karibuni umeibua msongamano kwenye huduma za umma na mamlaka ya Chad na  hawana uwezo wa kukidhi mahitaji ya wahamiaji pamoja na wananchi.

 Anne Kathrin Schaefer, Mkuu wa ofisi ya IOM nchini Chad amesema wahamiaji hao hawana chakula, maji na malazi stahili au hawana kabisa, na hata mamlaka ya Chad wala IOM hawana uwezo wa kifedha kukidhi mahitaji yao.

Wengi wa wahamiaji wasiojua la kufanya kwa sasa walitoka nchi jirani zikiwemo Burkina Faso, Niger, Nigeria, Sudan and Cameroon.