IOM yasaka dola milioni 2.1 kunusuru wasaka hifadhi walionasa Chad

6 Julai 2018

Shirika la uhamiaij la Umoja wa Mataifa, IOM, linasaka zaidi ya dola milioni mbili ili kukidhi mahitaji ya dharura ya wahamiaji waliokwama na walio kwenye vituo vya mpito nchini Chad.
 

Mkuu wa IOM nchini Chad Anne Kathrin Schaefer amesema fedha hizo zinahitajika kwa kipindi cha miaka miwili ijayo zinalenga pamoja na mambo mengine operesheni za kusaka na kuokoa wahamiaji kwenye maeneo ya kaskazini mwa Mali ambako wasafirishaji haramu wanazidi kuibuka na njia mpya ili kukwepa mbinu za udhibiti.

Amesema kuwa zaidi ya wahamiaji 100 wamekwama katika mji mkuu wa Chad, N’Djamena  ambapo 45 kati yao tayari wamepatiwa ushauri nasaha na wako tayari kurudi makwao endapo fedha zatapatikana

Ametaja eneo la Faya ambako biashara hiyo haramu imeshamiri, sambamba na mateso na utekaji nyara kwa wasaka hifadhi.

Watoto katika kitongoji cha wahamiaji Niamey Niger. Wengi wanaishi  huko baada ya kufukuzwa kutoka Algeria.
IOM Niger
Watoto katika kitongoji cha wahamiaji Niamey Niger. Wengi wanaishi huko baada ya kufukuzwa kutoka Algeria.

Halikadhalika fedha hizo zitatumika kusaidia wale wanaotaka kurejea nyumbani kwa hiari kwa kutumia njia ya anga na barabara.

Bi. Schaefer ameongeza kuwa watatumia sehemu ya fedha hizo kuanzisha kituo cha mapokezi ya wahamiaji huko Faya pamoja na kituo cha mpito kwenye mji mkuu  N’Djamena ambako  huduma kama vile za matibabu, kisaikolojia, chakula, maji na mapumziko zitapatiwa wahamiaji.

Sambamba na hilo amesema ni kampeni ya kuhabarisha wahamiaji kuhusu athari na hatari za uhamiaji unaokiuka kanuni pamoja na usafirishaji haramu wa binadamu.
 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter