Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waathirika wa mapigano ya kikabila Ethiopia wako hoi- IOM

Wakimbizi wa ndani- IDP- sehemu za Kercha,Zoni ya Guju Magharibi.
OCHA/ Tinago Chikoto
Wakimbizi wa ndani- IDP- sehemu za Kercha,Zoni ya Guju Magharibi.

Waathirika wa mapigano ya kikabila Ethiopia wako hoi- IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limetoa ripoti ya kina kuhusu  hali ya wakimbizi wa ndani watokanao na mapigano ya kikabila kwenye maeneo ya Gedeo na Guji magharib nchini Ethiopia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya wakimbizi wa ndani ni 958,175 ambapo mwezi uliopita ilibainika kuwa 359,113 kati yao wanaishi kwenye makazi 134 ya pamoja huku waliosalia huishi na jamii za wenyeji  au yaliyokodishwa na jamaa zao.

Mapigano kati ya jamii  hizo nchini Ethiopia yalianza tena mwezi Machi mwaka huu na maeneo ambako mizozano inaendelea ni kwenye eneo liitwalo Southern Nations, Nationalities People’s región -SNNPR- na lile la Oromo.

Uchunguzi uliyofanywa na IOM kwa ushirikiano na serikali ya Ethiopia ulibaini kuwa katika maeneo yote eneo la Guji magharibi ndilo lenye watu wengi waliokimbia hasa kutoka katika wilaya ya Kerca.

Katika eneo la Gedeo ambako ndiko idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani 970,000 wamesaka hifadhi kuna takribani watu 276,939 wanaoishi kwenye makazi 134 ya pamoja.

Baadhi ya makazi hayo ni shule, majengo ya serikali na pia majengo  ambayo hayajakamilika. IOM inasema katika maeneo saba, zaidi ya nusu ya wakazi wanaishi maeneo ya wazi wakati huu ambapo Ethiopia inakabiliwa na baridi kali na mvua.

IOM inasema kipaumbele hivi sasa ni kuwapatia makazi.

Nako sehemu za Guji Magharibi watu 82,174 wasio na makazi wanakaa katika makazi ya pamoja 43 ambapo matano kati ya hayo hayafikiki.

Wakimbizi hao walianza kufika makazi hayo mwezi Machi na hadi uchunguzi huu ulipofanyika mwezi Julai watu walikuwa bado wanawasili katika makazi hayo, licha ya kwamba hakuna vituo vya matibabu na njia ya kawaida za kupata chakula kwa familia zao.