Wahamiaji 8 toka Ethiopia wamefariki dunia wakiwa rumande katika hali mbaya Yemen:IOM

2 Mei 2019

Wahamiaji takriban wanane kutoka nchini Ethiopia wameripotiwa kufariki dunia nchini Yemen ambako walikuwa wanashikiliwa mahabusu kwenye vituo maalum, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM.

IOM imesema imetiwa hofu na taarifa za vifo vya wahamiaji hao rumande hasa kutokana na magonjwa yanayoweza kuzulika , lakini pia kwa kupigwa risasi, mateso na hali mbaya kwenye vituo wanavyoshikiliwa.

Vifo vya wahamiaji hao wanane vimeelezwa ni kutokana na magonjwa ya kuhara waliyoyapata kwenye kambi ya kijeshi ya Lahj inayoshikilia wahamiaji 1400 wengi wakiwa ni kutoka Ethiopia. Hali yao ilikuwa mbaya sana na walifariki dunia baada ya kufikishwa kwenye hospitali ya Khaldoon kwenye jimbo la Lahj.

Hivi sasa IOM inafuatilia kwa karibu hali ya wahamiaji 500 kutoka Pembe ya Afrika wanaoshikiliwa kwenye vituo vitatu ikiwemi katika viwanja viwili vya michezo, na kambi za kijeshi katika majimbo ya Aden, Lahj na Abyan.

 

Uongozi katika kambi hizi umearifu kubaini visa 200 vya kuhara na shirika la IOM linaanzisha kituo maalumu cha matibabu ya kuhara kwenye hospitali ya Ibn Khaldoon ambayo hkwa sasa inahaha kutibu wagonjwa 53 wenye ugonjwa wa kuhara wakiwemo wanane walio katika hali mbaya.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter