Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano ya kikabila Ethiopia yawaacha watu 970,000 bila makazi-IOM

Balanish Tadese, mmoja  kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya
UNHCR/Rose Ogola
Balanish Tadese, mmoja kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya

Mapigano ya kikabila Ethiopia yawaacha watu 970,000 bila makazi-IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Uchunguzi uliofanywa na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM unaonyesha kuwa  watu takriban 970,000 hawana makazi kutokana na ghasia za kikabila nchini Ethiopia.

Ripoti ya IOM iliyotolewa leo mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, inaeleza kama mapigano ya kikabila baina ya jamii zilizoko kwenye mpaka wa kusini mwa Ethiopia-SNNPR na katika eneo la Ogaden yamelazimisha watu kutoroka makwao  kuanzia mwezi Aprili mwaka huu na wengi kukimbia mwezi Juni pekee.

 Makadirio ya IOM, katika  ngazi za wilaya ,yaligundua kuwa  watu 822,187 walikimbia kutoka eneo la Gedeo ambalo ni la SNNPR na takriban 147,040 kutoka Guji magharibi ambalo ni eneo la kabila la waoromo.

 

Image
Bendera ya Ethiopia. Picha: UM/Loey Felipe

Lakini taarifa zinasema kikosi cha IOM kilichokuwa kinafanya uchunguzi hakikuweza kuwafikia watu wengine   walioko katika  wilaya nne kati ya sita katika eneo la Guji magharibi kutokana na hali ya usalama kuwa mbaya.

Taarifa inaongeza kuwa katika maeneo yote wakimbizi wengi wanakaa na jamii za mahali walipo mfano Gedeo watu zaidi ya 500,000, Guji magharibi zaidi ya watu elfu 84 na waliosalia wanakaa katika shule, vituo vya serikali, au magofu.

Miongoni mwao ni Mujib ambaye anaishi kwenye eneo lenye ukubwa wa mita nne kwa tano, eneo ambalo ni chafu na anaishi yeye na wakimbizi wengine 26 ikiwemo familia yake, Mujib ya watu wanane akiwemo mama yake mzazi.

“Eneo hili lina baridi sana, hatuna hata chakula cha kutosha, watoto wetu hawapati lishe sahihi. Sifahamu mazingira haya yatakuwa na athari gani kwenye maisha ya watoto wangu. Hili ni jambo gumu kufikiria hivi sasa,” amesema Mujib.

 

Image
Wakimbizi wa kutoka Ethiopia na Eritrea amabo wanaokolewa na wafanya kazi wa IOM.(Picha:© IOM 2015)

IOM inasema majengo yanayohifadhi wakimbizi hao wa ndani yamejaa kupita kiasi, baadhi wakilazimika kulala nje tena chini ya sakafu  bila kitu chochote cha kujifunika  isipokuwa turubaimoja tu  ambalo linawakinga  mvua.