Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 800,000 wanakabiliwa na baridi kali na mvua kubwa Ethiopia-IOM

Balanish Tadese, mmoja  kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya
UNHCR/Rose Ogola
Balanish Tadese, mmoja kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya

Watu 800,000 wanakabiliwa na baridi kali na mvua kubwa Ethiopia-IOM

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, limesema, zaidi ya wakimbizi wa ndani 800,000 nchini Ethiopia wanaishi bila makazi ya kutosha na huduma ya kujisafi na hivyo kusababisha kuzorota kwa hali ya kibinadamu inayochochewa na  baridi kali na mvua.

IOM katika taarifa kwa waandishi wa habari imesema, mapigano mwezi uliopita kati ya jamii za zilizopo mpaka wa mikoa miwili ya Ethiopia, ule wa maeneo ya kusini uitwao SNNPR na mkoa wa Oromia, yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makwao.

Shirika hilo limesema hao waliopoteza makazi mwezi uliopita, waliongeza kwa kiasi kidogo idadi ya waliofurushwa mwezi Aprili na Mei.

Watu walitembea kwa siku nyingi, wengi wakilala nje wakiwa safarini ambapo jamii zilizofurushwa hazina mali yoyote kando ya nguo walizovaa na wamebaki bila chakula au pesa.

Kwa mujibu wa takwimu za IOM kulikuwepo na wakimbizi wa ndani takriban milioni 1.7 kote Ethiopia kwa sababu ya ukame na mafuriko yaliyofuatia, kabla ya kufurushwa upya.

Taarifa ya IOM inasema watu walitembea kwa siku nyingi, wengi wakilala nje wakiwa safarini ambapo jamii zilizofurushwa hazina mali yoyote kando ya nguo walizovaa na wamebaki bila chakula au pesa.

Samira mwenye umri wa miaka 22 ni mama wa watoto saba amesema waliwasili miezi tatu iliyopita na sasa wanaishi katika eneo la Gedeb ambako mamlaka ya mitaa wameiomba IOM kuongeza msaada katika eneo.

Bi Samira ambaye alikimbia na wanae anasema licha ya ugumu wa hali yao anashukuru kwamba wamepata makazi akisema “tunashukuru kuwa tuna makazi lakini tunahitaji chakula zaidi na mavazi, watoto wetu wanahisi baridi. Kuna Mashirika ambayo yanatupa msaada lakini tunamahitaji zaidi."

IOM inashirikiana na serikali ya Ethiopia na tayari imewasilisha mablanketi 1,000 na hivi sasa imeanza ukarabati wa makazi 40. Pia imejenga vyoo miongoni mwa huduma nyingine.

Hata hivyo wakati mvua zikiendelea kunyesha, watu wanahitaji msaada na hivyo IOM imetolea wito jamii ya kimataifa kusaidia katika ufadhili.