Nina Imani na uwezo walio nao vijana:Guiterres

10 Agosti 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ana imani na uwezo walionao vijana katika kuleta mabadiliko duniani. Flora Nducha na tarifa zaidi

Katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya vijana Antonio Guterres amesema amani, uwezo wa kiuchumi, haki ya kijamii, uvumilivu yote haya na zaidi yanategemeana na kutumia uwezo walionao vijana si katika siku zijazo, bali leo na sasa hivi. Kwani hiyo ndio maana ya siku ya kimataifa ya vijana, na kusisitiza kuwa, "Vijana wanahitaji elimu na kupewa fursa, ajira bora, ushiriki kikamilifu,na sauti na kushiriki kwenye majadiliano. Nitahakikisha kwamba Umoja wa Mataifa unasikiliza sauti za vijana, unawawezesha na kufuata muongozo wao na Septemba mwaka huu tutaanzisha mkakati mpya wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana, tukiongeza juhudi zetu za kuwafanyia kazi na kushirikiana nao."

Naye mjumbe maalumu wa vijana kwenye Umoja wa Mataifa Jayathma Wickramanayake amesema vijana duniani wanahitaji fursa salama ambapo wanaweza kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi, na pia kufuata ndota zao iwe kwenye maeneo ya umma, ya kiraia au kwenye mitandao, kwani “Leo hii, zaidi ya vijana milioni 400 duniani wanaishi kwenye maeneo yaliyoathiriwa na vita au vurugu. Mamilioni wengine wanakabiliwa na unyanyasaji, ukatili na wengine haki zao kukiukwa na miongoni mwa walio hatarini zaidi ni wasichana na vigori, kama ilivyo kwa wakimbizi na wahamiaji vijana, wanaoishi kwenye sehemu zenye migogoro, na jamii ya vijana wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na wale waliobadilisha jinsia (LGBTQI)”.

Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa kwa kuifanbya dunia kuwa salama kwa vijana, tunaifanya dunia iwe bora kwa wote.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter